Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI David Silinde ameagiza uongozi wa Halmashauri za Wilaya katika mkoa wa Morogoro ambazo bado wapo nyuma katika ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kuhakikisha wanasimamia kwa karibu zaidi mafundi ili waweze kukamilisha kwa wakati katika muda ulioongezwa na Serikali ifikapo Disemba 30, 2021 ili kuruhusu wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza kuanza kutumia madarasa hayo.
Ametoa maagizo hayo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika halmashauri nne za mkoa wa Morogoro ambazo ni Gairo, Kilosa, Mvomero na Manispaa ya Morogoro na kukuta ni halmashauri moja tu ya Kilosa ndiyo iliyomaliza ujenzi kwa asilimia mia huku halmashauri ya Gairo ikiwa bado ipo nyuma wakiwa wanaezeka mabati katika majengo yao yote waliyopewa na kutaka waongeze spidi kwa kufanya kazi usiku na mchana kwani muda ulioongezwa ni mdogo kuliko kazi ambazo bado wapo nazo.
Ameongeza kuwa ametembelea halmashauri ambazo zipo mbali sana na viwanda vya saruji zinapozalishwa na vifaa vingine kama Katavi, Rukwa, Songwe lakini wamekamilisha majengo yao lakini inashangaza kuona mkoa wa Morogoro ambao upo karibu na viwanda vya uzalishaji wa vifaa bado upo nyuma kukamilisha kwa uharaka ujenzi wa madarasa na kutaka wakamilishe kwa wakati ikiwezekana kabla ya tarehe ya mwisho kwa ubora na thamani halisi ya fedha ionekane.
Kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja amesema sababu kubwa ya halmashauri ya Gairo kuwa nyuma katika ujenzi wa madarasa ni kutokana na kuagiza saruji Tanga ambapo walikuta foleni kubwa ya uhitaji wa bidhaa hivyo kuchelewa lakini wanaamini ndani ya muda ulioongezwa watakamilisha kwa wakati na halmashauri zingine ambazo zinakamilisha ujenzi huo.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa vyumba vya madarasa ambavyo sasa vitasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika chumba kimoja ambao walikua wanawaweka mpaka wanafunzi 100 kwa wakati mmoja lakini sasa watakaa wanafunzi 45 tu hivyo kufanya ufaulu kuongezeka.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa