Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaj Majid Hemed Mwanga amepiga marufuku wafugaji wote wa wilayani hapa kuacha kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao huku akiahidi kukomesha kukomesha tabia hiyo ambayo imekuwa ya muda mrefu.
Hayo yamejiri Julai 06 mwaka huu kwenye mkutano wa wadau wa kilimo na mifugo uliofanyika kwa lengo kuwakutanisha na kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili pande zote ambapo amesema kero kubwa ni wafugaji kulisha mazao ya wakulima na kusababisha hasara kwa wakulima huku fidia ikiwa haiendani na thamani ya mazao husika.
Mhe Majid Mwanga amesema kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni viongozi ngazi za vijiji kushindwa kusimamia sheria na miongozo iliyopo pamoja na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji kisha kuingiza mifugo kijijini hivyo amewataka watendaji kuwajibika kwa kuchukua hatua vitendo vinavyochochea migogoro kwenye jamii na wao wasiwe chanzo cha tatizo.
Mhe Mwanga amewaagiza watendaji kata kusimamia sheria ndogo ya mwaka 2014 ambayo inambana mfugaji kuhakikisha mifugo haizuruli na ukikamatwa mfugo mmoja ni shilingi elfu ishirini kwani sheria hiyo ilitungwa mahususi kwa ajili ya kuondoa adha hivyo wasimamie vema sheria hiyo ili kukomesha maatukio hiyo.
Aidha amemtaka OCD Kilosa kukamata mifugo yote inayozurula na kuiuza jambo ambalo litakomesha uingizaji wa mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kwamba suala hereni kwa mifugo ni agizo la Serikali ili kurahisisha utambuzi wa mifugo iliyopo katika wilaya hivyo wafugaji wahakikishe wanalikamilisha na hii itasaidia kukomesha tabia ya wizi na Afsa Mifugo atasimamia ili zoezi likamilike.
Hata hivyo amesema makundi ya wafugaji na wakulima ni makundi muhimu sana kwenye uchumi na maendeleo ya wilaya, hivyo ni lazima kwa Serikali kuchukua hatua pale ambapo kunahitaji nguvu aidha ya kimaendeleo au kuweka mambo sawa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa