Imeelezwa kuwa ipo haja ya kuendelea kutoa elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari kwani elimu hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi hao pindi wanapokuwa katika siku za hedhu na kuwa katika mazingira salama sambamba na kuendelea na masomo bila changamoto yoyote.
Anjelika Kira Afisa Lishe toka Worldvision amesema hayo wakati wa ugawaji wa taulo za kike takribani paketi 550kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Ukwiva na Zombo ambazo zina uwezo wa kutumika na kufuliwa kwa ajili ya matumizi ya kila mwezi ambapo lengo la ugawaji wa aina hiyo ya pad ni kuwasaidia kutoingia gharama za kununua kila mwezi ambapo amesema wanafunzi wengi wa kike wanapopevuka changamoto imekuwa ni namna ya kujihifadhi na vifaa vinavyotumika pindi wanapokuw akatika siku za hedhi.
Kira amesema asilimia kubwa kumekuwa na changamoto ya vifaa wanavyotumia kwani wengi wao wamekuwa wakitumia vifaa visivyo salama lakini pia vifaa hivyo baada ya matumizi vimekuwa vikihifadhiwa sehemu zisizo salama ikiwemo utupaji wa pad vyooni ama katika mashimo ya taka jambo ambalo si salama kiafya huku akisema kuwa hedhi salama ni hali ya matumizi ya vifaa salama katika mazingira salama na usiri ndani yake lakini pia kwa kuhifadhi pad hizo katika mazingira salama ambayo yatawawezesha kuhudhuria masomo yao kwa kipindi chote wanapokuwa shuleni.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Prisca Nivaco amewasihi wanafunzi hao kutofumbia macho suala la ukatili wa kijinsia kwa kuwa wazi pindi wanapotendewa vitendo vya kikatili ikiwemo ubakaji kwani kwa kufanya hivyo itasaidia jamii kubadilika dhidi ya vitendo vya kikatili huku Afisa Afya Ahobokile David akisisitiza suala la usafi wa mwili na mazingira ambapo amewataka kutumia taulo walizopewa katika hali ya usafi ili kujiepusha na magonjwa, michubuko, kuwashwa, fangasi na kutoa harufu mbaya pindi wawapo katika siku za hedhi.
Kwa niaba ya walimu wa shule zote mbili mwalimu Roida Mgina wa shule ya Sekondari Ukwiva ameushukuru uongozi wa Worldvision kwa ajili ya zawadi hiyo kwa wanafunzi huku akisema kuwa watakuwa karibu na wanafunzi kuhakikisha wanatumia taulo hizo inavyostahiki huku wanafunzi wa shule zote mbili wakitoa shukrani zao kwa kwani wanaamini zitawasaidia kukaa darasani kwa kujiamini na salama lakini pia kupitia mafunzo waliyoyapata wanaamini kiwango cha umakini darasani kitaongezeka sambamba na kuhudhuria masomo kila siku.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa