Katika juhudi za kuwaandaa wanafunzi kwa maisha ya baada ya shule, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na wamiliki wa vituo vya huduma ya maandiko (stationery), imeendesha mafunzo maalum kwa wanafunzi wa shule za sekondari Mazinyungu, Mbumi, Kutukutu na Dendego, yaliyofanyika jana katika shule ya sekondari Mazinyungu, wilayani Kilosa.
Afisa Mikopo kutoka HESLB, Bi Farida Mwasse, aliwafundisha wanafunzi hao kuhusu hatua za kuomba mkopo wa elimu ya juu, masharti ya kupata mkopo, pamoja na faida zake huku akibainisha kuwa mikopo hiyo inalenga kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kupata elimu ya juu kwa urahisi.
Kwa upande wake, Bi Graciana Mwinuka kutoka HESLB aliwaeleza wanafunzi kuwa kupata mkopo si tiketi ya ajira moja kwa moja, bali ni nyenzo ya kujiendeleza kielimu na kiujuzi na kusisitiza mkopo lazima ulipwe hata kama mhitimu hajapata ajira rasmi, hivyo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili wafanikishe ndoto zao, hasa wale wanaosomea masomo ya sayansi waliotajwa kuwa na kipaumbele.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Bi. Milandu Kinyonga, alipongeza juhudi za serikali kupitia HESLB kwa kuwafikia wanafunzi wa vijijini na kwamba ushiriki wa wafanyakazi wa stationaries katika mafunzo hayo ni wa muhimu kwani huwasaidia wanafunzi katika maandalizi ya nyaraka sahihi za kuomba mkopo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Mazinyungu, Mwl. Masegese Robert, alitoa shukrani kwa HESLB kwa kutoa elimu hiyo muhimu kwa wanafunzi, kwani yamewaamsha wanafunzi kuelewa namna wanavyoweza kusonga mbele kielimu bila kikwazo cha kifedha.
Kupitia mafunzo hayo, wanafunzi akiwemo Sadamu Augustino na Josephine Mlossa wameonyesha kufurahia elimu waliyoipata na kueleza kuwa sasa wana uelewa mpana kuhusu mchakato wa mikopo ya elimu ya juu na namna ya kujiandaa kimasomo ili kupata fursa hiyo muhimu ya kujikwamua kielimu na kiuchumi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa