Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mhe. Angelina Mabula amesema kuwa sekta ya ardhi ikiangaliwa kwa jichola karibu na kupewa kipaumbele ni moja ya maeneo ambayo yanaweza kiingizia mapato Serikali kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika ndani ya sekta hiyo ikiwemo malipo kwa ajili ya viwanja kwani sekta hiyo ni sekta mama na kwamba asilimia kubwa ya shughuli zote hufanyika kupitia ardhi.
Mabula amesema hayo Septemba 26 alipotembelea Wilaya ya Kilosa kwa ziara ya siku moja na kusema kuwa Idara ya Ardhi ikitelekezwa ni rahisi kuzaa migogoro ya ardhi kutokana na ufanisi wa kuwa chini, hivyo ni vema wakurugenzi wote nchini kila mmoja katika Halmashauri yake akatilia mkazo suala hili ili kuepuka migogoro ya ardhi ambayo si ya lazima lakini pia kutokuwepo kwa migogoro kutasaidia Halmashauri kuingiza mapato kwa urahisi na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi tunaopaswa kuwahudumia.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo amatembelea mashamba mbalimbali yakiwemo yaliyo na migogoro kama vile Farm Africa Agrofocus (T) Ltd lenye ukubwa wa ekari 13200.225, mashamba 6 yanayopendekezwa kufutwa Chanzuru yenye ukubwa wa ekari 1598 chini ya mmiliki Sadrudin Rajabal Meghji, mashamba mawili yaliyopo Kimamba shamba lenye ukubwa wa ekari 6945 chini ya mmiliki Sino Development Company na Sumagro Ltd lenye ukubwa wa ekari 7712 yote yakiwa hayajaendelezwa, pamoja na hayo kiongozi huyo na msafara wake walitembelea mashamba yaliyobatilishwa umiliki na mheshimiwa Rais yenye ukubwa wa ekari 8679 yaliyopo Mvumi na mwisho walitembelea mashamba pori yaliyotolewa notisi ya mwisho yakiwa Magole yenye ukubwa wa ekari 3507
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi alitumia fursa ya ziara hiyo ya Naibu Waziri kutoa ombi la mapendekezo la mashamba yanayopendekezwa kufutwa kwamba yawezwe kufutwa ili wapewe wawekezaji ambao wako tayari kwa ajili ya uwekezaji na kwamba kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza kipato kwa Halmashauri na kuleta maendeleo kiujumla katika wilaya nzima ikiwemo vijana kupata ajira kupitia uwekezaji utakaofanyika.
Aidha Afisa Mipango Miji na Vijiji Wilaya Masheka Mtatiro amesema Halmashauri inaweza kukusanya mapato kupitia ardhi kwa kukusanya kodi zote zitokanazo na ardhi kupitia mfumo wa Land Rent Management System (LRMS) na kupitia mfumo wa Government Electronic Payment Gateway (GEPG) makusanyo mengine yanaweza kukusanya kama vile kuhamisha ardhi, kuhuisha ardhi, ada ya upimaji nk.
Akihitimisha ziara yake Naibu Waziri ameitaka Idara ya Ardhi kuandaa taarifa ya kila robo mwaka itakayoonyesha wadaiwa sugu na hatua zilizochukuliwa, pia ametaka viwanja vyote ambavyo havijapimwa viweze kupimwa, uandikishaji wa hatimiliki ufanyike ili kuwasaidia wananchi kuwa na hati zitakazowasaidia na kuondoa migogoro, pamoja na kuandaa mpango kabambe ili ardhi itumike katika mpangilio sambamba na kuwataka watumishi wa Idara ya Ardhi kutokaa ofisini muda mwingi bali wawafikie wananchi na kuwahudumia inavyostahili huku wakishirikiana na Ofisi ya Kanda ili kuwasaidia katika changamoto mbalimbali zinazowakabili ili Kilosa iwe salama dhidi ya migogoro ya ardhi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa