Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha inawaletea wananchi maendeleo kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekusudia kujenga reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa hapa nchini ikiwa na upana wa mita 1435 reli ambayo inapatikana duniani kote kwa zaidi ya asilimia hamsini na tano.
Akielelzea kuhusu reli hiyo Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa Ismail A.Ismail amesema reli hiyo itakuwa ikipitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme na itakuwa na mwendo kasi usiopungua kilomita 160 kwa saa huku lengo la reli hiyo likiwa ni kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji nchini hususan katika sekta ya reli.
’’Miongoni mwa mambo yatakayorahisishwa kutokana na uwepo wa reli hiyo ni ongezeko la usafirishaji mizigo ambapo reli itabeba mzigo mpaka wa tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo, uokoaji wa muda kusafiri kwa abiria na mizigo, uboreshaji huduma za kijamii ikihusisha ujenzi wa shule, vituo vya afya na ujenzi wa barabara katika maeneo yatakayopitiwa na mradi pamoja na kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda’’. Ameongeza mhandisi
Aidha Ismail amesema ujenzi wa reli hiyo upo katika awamu tano ,awamu ya kwanza ni Dar es salam - Morogoro, ya pili Morogoro - Makutupora, awamu ya tatu Makutupora - Tabora, awamu ya nne Tabora - Isaka, awamu ya tano Isaka - Mwanza, ambapo awamu ya kwanza ilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Aprili 12 2017 na awamu ya pili Machi 14 2018.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ametoa rai kwa wananchi kutumia vizuri fursa ya uwepo wa mradi huo kwa kuchangamkia fusra za ajira na kibiashara zitakazojitokeza, kuchukua tahadhari ya magonjwa na kuwa wazalendo kwa kulinda mali zote za mradi ili kuhakikisha serikali ya awamu ya tano inatekeleza vema jukumu la kutuletea maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa