Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate Olenasha amewataka wanafunzi wote nchini wanaomaliza kidato nne pindi wamalizapo elimu hiyo kuishi maisha ya maadili na tunu waliyojifunza shuleni ili kuweza kukubalika katika jamii na kufanikiwa katika maisha yao ya sasa na hapo baadaye.
Olenasha amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 22 ya shule ya Sekondari Msolwa St. Gaspare Bertoni iliyopo kata ya Kisanga wilayani Kilosa ambapo amesema kumekuwa na hulka ya wanafunzi wanapomaliza kidato cha nne kuishi maisha yasiyofaa ya makundi mabaya jambo ambalo halistahili kwani wanafunzi hao wanapokuwa shuleni hufundishwa kuishi kwa maadili ambapo lengo la maadili hayo si kwa kipindi wanachokuwa wanafunzi bali ni kwa ajili ya maisha yao yote ili waweze kufanikiwa.
Olenasha ameongeza kusema kuwa serikali iko bega kwa bega na sekta binafsi hasa katika sekta ya elimu kwa kutoa ushirikiano ili kuhakikisha elimu na mafunzo yanayotolewa na sekta binafsi yanaendana na sera za awamu ya tano za kuwa na elimu bora itakayozaa wataalam wazuri na wasomi wenye kukidhi viwango vitakavyosaidia serikali ya Tanzania kiujumla.
‘‘Aidha niseme kuwa serikali ya awamu ya tano inatambua uwepo wa shule za binafsi na inaunga mkono juhudi zinazofanywa na sekta binafsi hasa upande wa elimu kwa kuweka mazingira wezeshi ili wawekezaji katika sekta ya elimu wawekeze katika mazingira mazuri pamoja na ushirikiano ili kupata watumishi wazuri wenye kuisaidia serikali na kuleta maendeleo’’ Ameongeza Olenasha.
Akieleza mafanikio yanayotokana na mpango wa elimu bure bila malipo amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiandikisha elimu ya msingi, ujenzi wa shule umeongezeka kutokana na uhitaji kuwa mkubwa, ongezeko la vitendea kazi kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi, mikopo imeendelea kutolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na waratibu elimu kata nchini kupatiwa pikipiki ili kurahisisha utendaji kazi na ufatiliaji wa maendeleo ya elimu kwa wanafunzi.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Mkurugenzi wa shule hiyo Bw. Godfrey Kolowoga amesema licha ya shule hiyo kuendana na changamoto za ukuaji wa sayansi na teknolojia hususani TEHAMA shule hiyo imefanikiwa kuwa na tovuti kwa lengo la kurahisisha mawasiliano na kupeana habari katika ulimwengu wa utandawazi, lakini pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafiri, uchache wa vyumba vya maabara kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo kwa masomo ya sayansi kwani haiwekani kuwa na wanasayansi wazuri wa baadaye pasipokuwa na maabara.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa