Jamii Wilayani Kilosa imetakiwa kuzingatia mwongozo wa Kitaifa wa chakula na ulaji ,ili kuondoa dhana potofu na mitizamo hasi iliyopo juu ya ulaji na ulishaji watoto ili kujenga familia yenye ustawi na afya njema.
Hayo yameelezwa Oktoba 30,2024 na Kaimu Afisa Lishe Wilaya ya Kilosa Elisha Kingu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa ambapo Kiwilaya yamefanyika katika kata ya Msowero kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Msowero.
Kingu amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuendelea kujengeana uwezo kuhusu masuala ya lishe na chakula kwa kufuata muongozo wa Taifa wa chakula na kwamba kuna makundi 6 ya chakula na yote yanapatikana katika maeneo mbalimbali wilayani hapa hivyo ameisisitiza jamii kula kwa kuzingatia makundi hayo angalau kila mlo uwe na kundi moja au mawili ya chakula.
Amesema kula kwa kuzingatia makundi hayo ya chakula kunasaidia kujikinga dhidi ya magonjwa lakini pia jamii itakuwa na nguvu ya kutimiza wajibu huku ikisaidia kumjenga mtoto akuwe katika hali nzuri,arefuke na kuwa na uzito unaofaa huku ufahamu wake ukiwa katika hali inayostahili hivyo kumuwezesha kufanya vizuri katika masomo.
Sambamba na hayo amesema kuwa ni muhimu kwa Mama mjamzito na familia nzima kwa ujumla kuhakikisha inapata chakula kinachokidhi mahitaji ya mwili ,huku akisistiza familia kuzingatia kutumia vyakula vyenye virutubisho vilivyoongezwa ikiwemo madini pamoja na Vitamini ili kupata virutubisho vya ziada na kujenga jamii yenye afya bora hivyo kuzalisha watu wenye uelewa mzuri kwa faida ya Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Afisa Afya Mbaraka Lilanga amewataka wananchi kutumia maji safi na salama kwaajili ya kunywa pia amewasisitiza kuhakikisha wanapika vyakula katika mazingira ya usafi ili kuepuka maradhi mbalimbali hususan magonjwa ya Milipuko.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii bi Leah Mayagi amewataka wakina mama kuzingatia kanuni za unyonyeshaji kwa kuhakikisha mtoto ananyonya kwa miezi sita bila kupewa chakula cha ziada kwani maziwa ya mama ni lishe iliyokamilika.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa