Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Mkinga ameitaka jamii kuendelea kutambua umuhimu wa ustawi wa mazingira kwa kuhakikisha kila mwanajamii anashiriki kikamilifu katika kutunza mazingira na kuyalinda kwa kushiriki katika mazoezi yote ya upandaji miti na utunzaji mazingira ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutunza na kustawisha mazingira.
Mkinga ameyasema hayo Aprili 13. 2024 wakati akiongoza kampeni ya upandaji miti katika shule ya Msingi Dumila Juu ambapo amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa katika kutunza mazingira na kuhakikisha nchi inakuwa katika ustawi bora hususani upande wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo ametaka kila mmoja kushiriki katika utunzaji wa miti inayopandwa katika maeneo mbalimbali huku akitoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa kuzingatia na kuifanyia kazi kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 isemayo ’’Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu‘‘ ambapo Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa na kukimbizwa wilayani Kilosa ifikapo tarehe 22/04/2024.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael J. Gwimile amesema zoezi la upandaji miti ni la msingi ambapo maelekezo ya Serikali kwa sasa ni uboreshaji mazingira ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo kwa sasa hali ya mvuai ni nyingi, hivyo ni vema watu wakazingatia kutokata miti na kufyeka mapori hovyo na badala yake kila mmoja aweke kipaumbele katika kuhamasisha upandaji miti jambo litakalosaidia kuwa na mazingira bora.
Mh. Deoglas Mwigumila ambaye ni diwani wa kata ya Dumila ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Kilosa kwa kufanya kampeni ya upandaji miti katika kata yake ambapo amesema wamejipanga kuwa mabalozi wazuri wa upandaji miti na kutunza mazingira huku akimshurkuru Mheshimiwa Rais kwa ajili ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Misungi ambayo inatarajiwa kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru na kwamba shule hiyo ni msaada mkubwa kwa wanafunzi kusoma kwa nafasi.
Naye Kaimu Mhifadhi Misitu TFS Bi.Hilda Mwalongo amesema kwa mwaka 2023/24 Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ilitoa Malengo ya Kitaifa kila Wilaya kupanda miti laki moja na nusu (1,500,000) ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni kampeni shirikishi ambapo mpaka sasa wilaya ya Kilosa jumla ya miche ya miti 1,389,466 kati ya 1,500,000 imepandwa sawa na 92.63% huku zoezi likiwa ni endelevu.
Aidha amesema ipo mikakati ili kufanikisha lengo ikiwemo kutoa Elimu ya Mazingira kwa jamii, Kuanzisha klabu za Mazingira mashuleni, Kushirikisha jamii kwenye masuala ya Mazingira, Kuunda, kusimamia na kuboresha kamati za maliasili zilizopo, kuendelea kutoa elimu ya uchomaji moto na kutunza vyanzo vya maji, kuendelea kushirikiana na Wadau wa Mazingira kwenye masuala ya kimazingira, kuhamasisha Serikali za vijiji kusimamia kikamilifu miti iliyopandwa na Misitu iliyopo, Kuweka ulinzi kwenye vyanzo vya maji kwa kushirikiana na mamlaka za maji na bonde sambamba na kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya upatikanaji wa vitendea kazi katika vitalu vya miche.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa