Mwenyekiti wa Kamati Shirikishi ya Kudhibiti Ukimwi Wilaya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Hassan Kambenga amevitaka vikundi mbalimbali vya watu wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutambua mchango unaotolewa na Halmashauri kwa kuhakikisha vinahamasisha jamii kupima afya zao.
Kambenga ametoa rai hiyo Mei 19 mwaka huu wakati alipokuwa akifungua kikao kilichokuwa kinalenga kufanya uchaguzi wa viongozi wa baraza la watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wilayani Kilosa ambapo amesema zipo faida mbalimbali za jamii kupima na kujua afya zao ikiwemo kujua tatizo na kupata tiba mapema ambapo amewataka washiriki wa kikao hicho kuendelea kuhamasisha jamii kupima afya mara kwa mara na kuchukua hatua stahiki.
Kambenga amesema kwa upande wa vikundi vya watu wenye VVU ni rahisi kupata sapoti toka serikalini na Halmashauri kiujumla sambamba na kupata misaada ya kiuchumi ambapo amesema vikundi hivyo vinahitaji kuwa hai badala ya kudorora ambapo kwa sasa vikundi vilivyo hai wilayani Kilosa vipo 10 kati ya vikundi 24 vinavyotambulika jambo linalopelekea hali ya utendaji kazi katika kuvihudumia vikundi hivyo kuwa ngumu kutokana na kudorora kwa vikundi hivyo.
Akizungumzia upande wa mradi wa Hebu Tuyajenge Kambenga amesema mradi huo unatarajiwa kufanya kazi katika kata tano zenye hali ya juu ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambapo upande wa viongozi watakaochaguliwa amewataka kuiga mfano mzuri wa viongozi waliopita lakini pia kuhamasisha vikundi vilivyodorora kuinuka upya, kuhamasisha jamii kupima afya lakini kusimamia uanzishwaji wa vikundi vipya ili viweze kupata sapoti kutoka Halmashauri.
Akizungumzia uwepo wa mradi wa Hebu Tuyajenge Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Bi. Sophia Liundi amesema mradi huo ni mradi wa miaka mitano ambao unaofadhiliwa na Shirika la Watu wa Marekani USAID ukiwa na lengo la kuongeza mapambano ya kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI nchini Tanzania ambapo wilayani Kilosa unatarajiwa kufanya kazi katika kata tano za Rudewa, Dumila, Mikumi, Kasiki na Kidodi.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Rwegerera Katabaro pamoja na Mratibu wa UKIMWI Wilaya Merrisiana Temu kwa pamoja wameushukuru uongozi uliopita kwa kazi kubwa waliyofanya kwa kipindi chao cha uongozi huku wakiwataka viongozi wateule kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo ili kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa imara kwani Halmashauri ipo kwa ajili ya kuwasaidia na kuwapa sapoti ili waweze kusonga mbele.
Katika uchaguzi huo uliochagua viongozi kwa ngazi mbalimbali umefanikiwa kumchagua Rashid Namtuka kwa nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mweneykiti akiwa ni Mariana Lucas, Zuhura akiwa Katibu, Mweka hazina Rehema Seif na viongozi wengineo ambao watakuwa wakishiriki katika vikao vya Kamati Shirikishi ya Kudhibiti Ukimwi Wilaya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa