Kufuatia kauli mbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2021 isemayo ‘’Zingatia Usawa, Tokomeza UKIMWI , Tokomeza magonjwa ya mlipuko’’ wananchi wilayani Kilosa wamesisitizwa kuzingatia suala la usawa kuanzia ngazi ya kaya katika masuala ya afya ikiwemo upimaji wa hiari wa virusi vya ukimwi(VVU) na magonjwa ya mlipuko ikiwemo COVID.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawal a Wilaya Yohana Kasitila kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo huadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka ambapo usawa ukizingatiwa na upimaji wa hiari itasaidia kupunguza kiwango cha maambuziki mapya ya VVU na UKIMWI katika jamii na kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.
Aidha amesema kuwa ugonjwa wa UKIMWI umeleta athari mbaya kwa jamii na kiuchumi na kuleta hali ya umaskini na migogoro ya kifamilia kwa jamii, vifo vingi na kusababisha uwepo wa yatima lakini pia unachangia kupoteza nguvu kazi , kupunguza uzalishaji mali na kuongeza gharama za tiba na huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI ambapo matokeo yake ni kuathiri kasi ya ukuaji na ustawi wa uchumi wa wilaya na watu wake.
Naye Mratibu wa UKIMWI Wilaya Merrisiana Temu amesema kufikia mwezi Oktoba, 2021 mwenendo wa maambukizi kati ya watu waliojitokeza kupima 2.9% ya watu wote waliobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kiujumla inaonyesha maambukizi kati ya watu wanaojitokeza kupima yanapungua mwaka hadi mwaka.
Temu amesema vichocheo vya maambukizi kiwilaya ni uwepo wa barabara kuu na maegesho ya magari makubwa katika maeneo ya Mikumi na Dumila, kuwepo kwa maeneo ya kibiashara ya mazao na uwepo wa ujenzi wa reli ya mwendo kasi na miundombinu ya barabara ni miongoni mwa maeneo ambayo hukutanisha watu wa aina mbalimbali hivyo kupelekea mahusiano ya kingono na biashara ya ngono.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa