Katika kuendesha kampeni maalum ya utoaji elimu na chanjo ya UVIKO 19 ndani ya siku 14 ya nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa inayoendelea nchi nzima kuanzia Oktoba 1 hadi 14 mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Majid Mwanga ametoa rai kwa wananchi kujikita zaidi kwa kuwasikiliza wataalam wa afya ili kupata elimu ya pamoja juu ya UVIKO 19 badala la kujikita zaidi katika kutafiti kupitia mitandao ya kijamii.
Mwanga ametoa rai hiyo Oktoba 6 mwaka huu wakati wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Chanjo ya UVIKO 19 ambapo ameitaka kamati hiyo kupata elimu ya pamoja juu ya ugonjwa huo ambapo ametaka kufuatwa kwa masharti na ushauri unaotolewa na wataalam ili kuwa msaada kwa jamii isiyo na uelewa juu ya UVIKO 19.
Aidha ameitaka kamati hiyo kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kuisaidia jamii kila mmoja katika eneo lake kwani chanjo ni salama na kwamba suala la upotoshaji katika jamii halikosekani, hivyo kila mmoja awe mfano katika kuhamasisha wale ambao hawajapata chanjo ili waweze kupata chanjo ili kuwa salama kiafya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba amesema chanjo ya UVIKO 19 ni muhimu kwa kila mmoja kwani kati ya changamoto za maradhi zilizopo mojawapo ni UVIKO 19 hivyo Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wake wanapata chanjo kwa kuhakikisha elimu ya umuhimu wa chanjo inatolewa kwa wananchi ikiwa imeambatana na shughuli za uchanjaji hivyo kupitia kamati hiyo anaamini hamasa itafanyika ya kutosha ili kutoa elimu.
Pamoja na hayo amesema Halmashauri imejipanga vizuri kuhakikisha jamii inafikiwa na kupata elimu pamoja na chanjo huku akisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amekuwa mhamasishaji mkuu kwa jamii kupata chanjo kwani chanjo ni salama hivyo Halmshauri iko tayari kufika maeneo yote ili kutoa elimu na chanjo lengo ikiwa ni kupunguza maambukizi.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Dkt. George Kasibante amesema kwa sasa vituo vyote vinatoa huduma ya chanjo ya korona tofauti na awali ilipoana huduma ya utoaji chanjo ilikuwa ikitolewa katika vituo vitatu tu na kwamba lengo la utoaji chanjo dhidi ya UVIKO-19 ni kupambana na ugonjwa huo unaozuilika kwa chanjo, Kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Korona, Kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo huku akisema kuwa unafanyika uhamasishaji kwa lengo la kuhakikisha kuwa jamii inahamasika na kuelewa umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 ili kupata ushirikiano na kuchanja.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa