Katika kuhakikisha misitu iliyopo katika Wilaya ya Kilosa inatunzwa na kudhibitiwa dhidi ya vitendo vya moto vinavyojitokeza katika misitu ya vijiji kwa ajili ya matumizi mbalimbali jamii zinazoishi kuzunguka misitu hiyo zimeshauriwa kuhakikisha misitu hiyo inatunzwa katika hali ya uendelevu kwa kushirikiana na TANAPA ili kuhakikisha kunakuwa na hali ya uendelevu.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba wakati wa ziara ya kutembelea misitu vijiji katika kijiji cha Kitunduweta kwa lengo la kujionea namna kijiji hicho kinavyotunza misitu katika hali ya uendelevu licha ya shughuli za uvunaji mkaa na mazao mengine ya misitu kuendelea.
Kisena amesema ipo haja ya vijiji vyenye misitu na uongozi wa vijiji husika kukaa kwa pamoja na TANAPA na kuweka mikakati ya pamoja ili kuhakikisha shughuli za uchomaji moto zinafanyika kwa usahihi katika kuhakikisha misitu hiyo inakuwa salama na endelevu jambo litakalosaidia udhibiti wa moto.
Akizungumzia kero ya ng’ombe kuingia kwenye mashamba na kutochukuliwa hatua zozote kwa kisingizio cha ng’ombe wa viongozi wa juu amesema suala hilo si sahihi na linapaswa kuchukuliwa hatua na viongozi wote kuanzia ngazi ya chini kwa kulidhibiti ili kutoleta migogoro huku akiwataka wananchi kutosita kutoa taarifa endapo hatua stahiki hazitachukuliwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila ameshauri vijiji vyenye misitu hususani kijiji cha Kitunduweta kuwa mfano bora wa kutekeleza mipango mbalimbali iliyojipangia ili kuleta matokeo chanya ikiwemo utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi, mpango wa uvunaji pamoja na mpango wa matumizi ya rasilimali za misitu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa