Mratibu magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele Wilaya Bi.Rose Nguruwe amebainisha kuwa magonjwa ya trakoma, usubi, kichocho, minyoo, matende na mabusha ni magonjwa ambayo yanadhibitiwa na mpango wa Taifa kwa kutolewa madawa katika maeneo mbalimbali hususani mashuleni kwenye kaya kama kinga lakini pia hutolewa kwa wagonjwa ambao tayari wameshaathirika na magonjwa hayo..
Akifafanua magonjwa hayo Agosti 27 mwaka huu katika kikao uhamasishaji kilichoshirikisha viongozi wa dini, viongozi wa siasa na wakuu wa idara na vitengo Rose amesema kuwa upande wa ugonjwa wa kichocho huenezwa kupitia binadamu kwa kueneza vimelea vya ugonjwa kwa njia ya kujisaidia katika vyanzo vya maji ambapo vimelea hivyo huingia kwenye konokono kwenye maji yaliyotuama ambapo husababisha damu kutoka kwenye mkojo na kinyesi na baadae inaweza kusababisha saratani ya tumbo, kibofu cha mkojo na ini.
Kwa upande wa minyoo ya tumbo huathiri zaidi jamii maskini ambapo huambukizwa kwa kula mayai ya minyoo na namna ya kujikinga ni kwa kutumia dawa za minyoo na kuongeza kiwango cha usafi.
Nguruwe amesema mabusha na matende husababishwa na minyoo midogo inayoathiri mfumo wa maji na huenezwa na mbu wa aina zote kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ambapo amesema kuwa matibabu yanatolewa hivyo mgonjwa afike hospitali kupata matibabu,na ameshauri matumizi ya vyandarua muda wote sambamba na kutunza mazingira ili kuepeusha mazalia ya mbu.
Akielezea usubi ni nini, amesema ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo ya filaria aina ya Onchecerca Volvulus na kusambazwa na inzi weusi wadogo wa kike wajulikanao kama Simulium ambao huzaliana kwa wingi kwenye maeneo yenye vijito/mito yenye maji yanayotiririka kwa kasi.
Licha ya uwepo wa magonjwa hayo Muuguzi Mkuu Wilaya Bi Mwanaisha Chitanda amesema kuwa magonjwa hayo yanatibika na kwamba ipo haja ya jamii kutumia kinga tiba na kwamba dawa hizo ni salama na hazina matatizo yoyote hivyo ni vema jamii ikahamasishwa kutumia kinga hizi ili iweze kumeza dawa kwa wingi ambapo dawa hizo hutolewa katika kaya , vibanda Maalum, makundi maalum mfano walemavu na kwamba katika suala zima la utoaji dawa huzingatia uzito na umri ambapo huanza kutolewa kwa watoto kuanzia miaka mitano.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa