Wito umetolewa kwa viongozi mbalimbali na wananchi kiujumla kuendelea kuiishi kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru katika maeneo yao kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa ipaswavyo kwa maslahi mapana ya uhai wa viumbe hai pamoja na uchumi wa taifa kwani kumekuwepo na mabadiliko ya tabianchi ambao umesababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu.
Hayo yamebainishwa Mei 17 mwaka huu na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh.Wilfred Sumari katika kikao cha baraza la Madiwani ambapo amesema kuwa kupitia mabadiliko ya tabianchi ipo haja ya wilaya kuendelea kuiishi kauli mbiu hiyo kwa kila mmoja kwa kutunza mazingira kwani vyanzo vya maji vimeendelea kukauka lakini pia kumekuwepo na hulka ya baadhi ya watu kuchafua vyanzo vya maji jambo ambalo si sahihi.,
Akizungumzia suala la mapato amesema ipo haja ya halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vya mapato vyenye uhakika ili kuinua mapato ya halmashauri kwa kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kujenga stendi za mabasi na maegesho ya malori mikumi na dumila,Sambamba na hayo Mh Sumari amewataka watendaji wa idara mbalimbali za Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato vya uwakika ambavyo vitakuwa mali ya kilosa kwa ajili ya kuongeza ukusanyaji wa mapato yatakayosaidia kuboresha huduma na shughuli mbalimbali za kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Kilosa
Pamoja na hayo ameishukuru uongozi wa Rais wa awamu ya sita Mh Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa shilingi Bilioni 2,025,800 kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi Tanzania (BOOST) ambapo fedha hizo zitasaidia kujenga shule, vyumba vya madarasa na vyoo hivyo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba amewaomba madiwani wa kata kushiriki kikamilifu katika usimamizi na utekelezaji wa mradi wa BOOST ambapo ametaka kuwepo na hali ya uhakiki na kijiridhisha kwa bei za vifaa na uletwaji wa bidhaa za ujenzi katika maeneo yatakapofanyika miradi ya BOOST jambo litakalosaida kutokiukwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo lakini pia utapelekea miradi hiyo kufanyika kwa ubora wa thamani ya fedha.
Aidha ametoa rai ya usimamizi wa miradi mingine inayoendelea katika kata mbalimbali ikiwemo miradi katika sekta ya elimu, afya na mingineyo kuwe na usimamizi wa matumizi ya fedha ambapo zinapaswa kutumika ipasavyo kwa kufuata taratibu ili kujiepusha na suala la uwepo wa fedha za bakaa lakini pia amesisitiza suala la ushirikiano na umoja katika kuiendesha halmashauri hususani katika suala la ukusanyaji wa mapato katika vyanzo mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa