Katika kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi Jumuiya ya Wazazi Wilaya imedhimisha maadhimisho hayo kwa kufanya ziara ya kuwatembelea watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mazinyungu ambapo wamekutana na watoto hao na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Akizungumza katika ziara hiyo Katibu wa CCM Wilaya Shaban Mdoe amesema lengo la ziara hiyo ni kuonyesha umuhimu wa watoto hao katika jamii kwani ni kama watoto wengine ambao wanapaswa kuonyeshwa upendo ambapo amesema kutokana na idadi ya wanafunzi hao wapatao 96 eneo wanalotumia kwa malazi halitoshi hivyo ipo haja ya kuongeza majengo mengine ili waweze kukaa vizuri.
Aidha amemshkuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akiwajali watoto kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ikiwemo fedha za chakula ili kuwawezesha kupata elimu yao ambapo pia amesisitiza jamii kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum kwani katika juhudi za kuinua kiwango cha elimu, nchi nzima imewezeshwa kwa kupatiwa fedha zilizowezesha kujengwa madarasa ili watoto waweze kupata elimu.
Pamoja na hayo amewasisitiza watoto hao kutojiona wanyonge kwani licha ya ulemavu walionao lakini wana uwezo wa kusoma na kupata maarifa ambayo yatawasaidia katika maisha yao kwani kila mmoja ana kipaji chake ambacho Mungu amemkirimia na kwamba wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika maisha yao.
Akibainisha zawadi walizojaliwa kuwapatia watoto hao Katibu wa Jumuia ya Wazazi Wilaya Bi Scholastica Salim amesema wamefanikiwa kuwapatia magunia mawili ya mkaa, sabuni za mche boksi moja lenye miche kumi, sabuni ya unga mmoja wa kilo 25 pamoja na mafuta ya kupakaa dazani 4 huku Mkuu wa shule hiyo Kajika Gallani ameushukuru uongozi wa CCM Wilaya kwa kuwakumbuka na kuwatembelea ambayo kwao ni faraja kubwa na wamejisikia kufarijika mno.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa