Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ikiongozwa na Makamo mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Hassan S. Mkopi imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kamati hiyo imetembelea miradi kuanzia tarehe 30-31Oktoba, 2024 ambapo imeipongeza Timu ya menejimenti kwa hatua iliyofikia na kuitaka kuendelea kusimamia vema utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mhe. Mkopi ameridhishwa na utekelezaji wa miradi na kushauri timu ya wataalamu kwa kushirikiana na wasimamizi wa miradi kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati.
Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Ukarabati wa hospitali ya wilaya ambapo jumla ya majengo 13 yatakarabatiwa. Ujenzi wa jengo la Maabara umeanza mradi upo hatua ya upauaji unaogharimu kiasi cha shilingi 315,677,050 kukamilika.
Pia kamati hiyo ilitembelea ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo katika shule ya Sekondari Rudewa mradi huo upo hatua ya umaliziaji unaogharimu kiasi chaShilingi146,400,000 fedha kutoka serikali kuu.
Aidha kamati ya fedha ilitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo katika shule ya sekondari Gongwe ujenzi upo hatua ya umaliziaji ambapo kiasi cha shilingi 190,400,000 fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya maendeleo ya elimu nchini Sambamba na umaliziaji wa Zahanati ya Mfulu ambapo shilingi 50,000,000 zimepokelewa kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo.
Vilevile kamati ya fedha ilitembelea ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo katika shule ya sekondari Mati pamoja na ujenzi wa chumba 1 cha madarasa na matundu 8 ya vyoo katika shule ya sekondari Masanze.
Katika hatua nyingine kamati ya fedha ilitembelea na kukagua ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo katika shule ya sekondari Zombo pamoja na kituo cha Afya Ulaya ambapo kituo hicho kipo hatua ya upauaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa