Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ikiongozwa na mwenyekiti wake Mhe. Denis Lazaro Rondo ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mikumi imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya “BOOST na SEQUIP” wilayani Kilosa ilipotembelea miradi hiyo Februari 20, 2024.
Akizungumza kwa niaba ya kamati, Mhe. Londo amezipongeza kamati za ujenzi katika miradi hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi wa miradi hiyo.
Kamati hiyo imetembelea na kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Miwa iliyopo katika kata ya Ruhembe amabayo imejengwa kwa kiasi cha shilingi 528,998,425.00 kwa ajili ya vyumba vya madarasa 8, jengo la utawala 1, maabara 3 ya kemia, bailojia na fizikia, maktaba, chumba cha Tehama, matundu ya vyoo 11, kichomea taka na tanki la maji la ardhini. ambayo imekamilika na imeshaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa upande wa mradi
Aidha kamati hiyo pia umekagua mradi (BOOST) ujenzi wa shule ya Msingi Ruaha A iliyopo katika kata ya Ruaha uliogharimu kiasi cha shilingi (98,000,000) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 4 na matundu 6 ya vyoo.
Mhe. Rondo amesema kuwa mradi wa ujenzi wa sekondari mpya ya Miwa imekuwa mkombozi kwa wanafunzi waliokuwa wanatembea zaidi ya kilometa 20 kwenda shule ya jirani kusoma kwani wanafunzi wengi wamekatishwa ndoto zao za kusoma kutoka na vikwazo walivyokuwa wanakutana navyo njiani huku wengi wakibakwa na wengine kupata mimba.
Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha shilingi 528,998,425.00 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo pamoja na miradi mingine ndani ya kata hiyo kama vile ujenzi wa Daraja Ruhembe linalojengwa kwa thamani ya shilingi zaidi ya bilioni moja.
Naye mbunge wa jimbo la Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewaasa wananchi wa Ruhembe kuitunza miundombinu ya shule hiyo huku akiwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwani miondombinu na mazingira ya shule hiyo ni rafiki kwao kujipatia elimu iliyo bora.
Pia mbunge wa viti maalum kutoka mkoa wa Tabora Mhe. Hawa Subira Mwaifunga ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo amewataka watendaji kusimamia vizuri miradi mbalimbali inayoendelea kutekelewa wilayani humo.
Sambamba na hayo Mbunge wa jimbo la Hai Mhe. Sashisha Herinikyo Mafue ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo amewapongeza wananchi wa jimbo la la Mikumi kwa kumchagua Mhe. Rondo kuwa mbunge wao kwani amekuwa msaada mkubwa kwa jimbo hilo na serikali kwa ujumla hususani katika kuiongoza kamati hiyo kwa weredi mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameishukuru kamati hiyo kwa kuitembelea wilaya ya Kilosa na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali huku akiwaahidi wanakamati na wananchi kwa ujumla kuendelea kuitunza miradi hiyo Pamoja na kuisimamia miradi mingine inayoendelea kutekelezwa wilayani humo.
Aidha mh. Shaka ameahidi kuwa hatowafumbia macho baadhi ya watendaji, wahandisi pamoja na wakandarasi wataoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika ujenzi na usimamizi wa miradi hiyo kwani serikali ya awamu ya sita imejizatiti kuwaletea huduma wananchi wake.
Akihitimisha ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo amabaye pia ni mbunge wa jimbo la Kilolo mkoani Iringa Jastin Lazaro Nyamoga ametoa pongezi kwa wasimamizi wa miradi hiyo akiwemo mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kuisimamia miradi hiyo kwani inakidhi ubora unaotakiwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa