Katika kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya chama tawala (CCM) inatekelezwa katika ngazi ya wilaya Kamati ya Siasa Wilaya imetembelea miradi mbalimbali katika jimbo la Kilosa na Mikumi ili kujionea namna ilani hiyo inavyotekelezwa katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Kamati hiyo imefanya ziara ya siku mbili katika jimbo la Kilosa na Mikumi Aprili 22 hadi 23 mwaka huu ambapo katika imetembelea miradi katika sekta ya elimu, maendeleo ya jamii, maji na afya ambapo imepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa Halmashauri pamoja viongozi wa kata kwa namna ambavyo wameshirikiana sambamba na wananchi katika kujiletea maendeleo.
Akiongelea miradi iliyotembelewa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilosa Abdallah Mdimu amesema wamejionea kazi kubwa iliyofanywa huku wakipongeza kuwa miradi hiyo inalingana na kiwango cha thamani ya fedha kilichotumika ambapo pia amesisitiza watumishi wote katika sekta hizo kufanya kazi kwa uzalendo kwa ajili ya taifa lao.
Aidha kamati hiyo kwa imepongeza juhudi kubwa zilizofanywa katika kituo cha afya Mikumi kwa huduma kubwa mbili za upasuaji zilizopelekea kuokoa maisha ya mama na mtoto ambazo zilifanyika kwa ufanisi na ushujaa mkubwa huku wakisisitiza kuwepo kwa uzio katika vituo vyote vya afya ili kulinda mipaka huku upande wa elimu wakitaka shule zilizotembelewa kuwa na mpango wa mabweni kipaumbele kikiwa kwa watoto wa kike ili kuwaepusha na vishawishi wanavyoweza kukumbana navyo ikiwemo mimba.
Pamoja na hayo kamati hiyo imeitaka Halmashauri na idara husika kuvisimamia kwa ukaribu vikundi vyote vilivyochukua mikopo na bado havijarejesha kuhakikisha vinafanya hivyo ikiwemo kuvisaidia kwa kuvisimamia ili vitumie mikopo hiyo kikamilifu na kitaalam kwa lengo la kupata tija na kurejesha fedha ili vikundi vingine viweze kukopa huku wakisisitiza vikundi vilivyokopa kurejesha mikopo kwa wakati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Adam Mgoyi amemuagiza mtendaji wa kata ya Ruaha kukisimamia kikundi cha walemavu kilichopo katika kata ya hiyo kwa kuhakikisha kinavuniwa miwa yake ambayo ipo tayari kwa kuvunwa ili kivuniwe na kufanya mauzo ambayo yatakiwezesha kupata fedha na kuanza kurejesha mkopo ambao kimepatiwa na Halmashauri kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Katika ziara hiyo miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati imetembelewa katika ni shule za sekondari Mikumi, Ukwiva, Dakawa na Kilosa, shule za msingi za Lumango, Ujirani, Msowero na Matongolo huku upande wa maendeleo jamii vimetembelewa kikundi cha walemavu kilichopo katika kijiji cha Kifinga, kikundi cha kinamama Mvumi na kikundi cha vijana kinachojishughulisha na mradi wa kutengeneza chaki kilichopo kata ya Magole na upande wa afya kituo cha Afya Mikumi, Dumila na Mvumi pamoja na mradi wa maji uliopo kata ya Kitete.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa