Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kilosa imemzawadia OC CID wa Wilaya ya Kipolisi ASP Onesphory Lesio zawadi ya shilingi 100,000/ ikiwa kama pongezi kwake kwa kitendo cha uzalendo na kishujaa alichokionyesha kwa kukataa rushwa ya shilingi 340,000/= toka kwa watuhumiwa ambao kesi yao ilikuwa mahakamani ili awasaidie na kuwaachia baada ya kukutwa na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
MKUU WA WILAYA AMBAYE NI MWENYEKITI WA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WILAYA ADAM MGOYI AKIMKABIDHI OC CID ONESPHORY LESIO ZAWADI YA SHILINGI 100,000/
Zawadi hiyo imetolewa Aprili 9 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi Aprili 8 tukio hilo lilishuhudiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo Mkuu wa Wilaya amesema OC CID huyo ameonyesha kitendo cha uzalendo kwani kwa nafasi yake alikuwa na nafasi nzuri ya kupokea rushwa hiyo lakini kutokana na kuithamini kazi yake hakupokea rushwa ambayo inapoteza haki za watu na kusababisha uonevu ambapo OC CID huyo baada ya ushawishi huo wa kupokea rushwa alitoa taarifa kwa taasisi ya kupambana na rushwa (TAKUKURU) ambao walifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa baada ya kuweka mtego uliowanasa watuhumiwa.
Mgoyi amesema kuwa kitendo kilichofanywa na OC CID ni kitendo cha uzalendo kwani Wilaya ya Kilosa imekuwa ni mhanga wa matendo ya rushwa lakini kutokana na mabadiliko ambayo viongozi wamekuwa wakionyesha kwa kukemea vitendo vya rushwa kwa vitendo hivyo kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuunga mkono kitendo cha kizalendo imemzawadia kiasi hicho cha fedha huku akisema mfano huo uwe ni wa kuigwa kwani anaamini jeshi la polisi ni chombo chenye uadilifu hivyo waige kutoka kwa kiongozi huyo na kwamba kila mwananchi anaowajibu wa kumuunga mkono Rais wa awamu Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupinga vitendo vya rushwa.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kilosa Lawrance Mlaponi amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa OC CID walifanikisha kuwakamata watoa rushwa na kwamba TAKUKURU inatoa wito kwa watumishi wa umma kutojihusisha na vitendo vya rushwa ili kutotekeleza majukumu yao huku akisisitiza wananchi kutotoa rushwa kwa watumishi ili kupata haki wasiyostahili ama upendeleo na kwamba yoyote anayejihusisha na masuala ya rushwa TAKUKURU haitasita kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola.
OC CID ONESPHORY LESIO AKISHUKURU KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WILAYA YA KILOSA.
Akielezea tukio hilo OC CID ASP Onesphory Lesio amesema watuhumiwa baada ya kuona kesi yao iko mahakamani na ndugu zao wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola walikusudia kutoa rushwa ili aweze kuwasaidia ambapo kutokana na uzalendo na uadilifu alitoa taarifa TAKUKURU ambao walitoa ushirikiano na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa pia amesema anawashukuru TAKUKURU kwa namna walivyotoa ushirikiano na kusema kuwa Jeshi la Polisi limedhamiria kupinga vitendo hivyo kwani awali Jeshi la Polisi lilikuwa likikataa vitendo vya rushwa pasipo kukamata wahusika lakini kwa sasa linakemea vitendo hivyo kwa kuhakikisha wanawakamata watuhumiwa kwa kuwashirikisha TAKUKURU hivyo kila mmoja ashiriki kwa nguvu zote kukemea vitendo vya rushwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa