Imeelezwa kuwa serikali kwa kiasi kikubwa imeweza kuweka mifumo mbalimbali ya utoaji huduma za afya na ustawi wa jamii zikiwemo kamati shirikishi za ukimwi katika jamii na kamati mbalimbali licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa fedha na mafunzo na kusababisha kutofikia malengo yaliyokusudiwa.
Hayo yameelezwa na Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Ukimwi Mkoa Bi. Ndayakundwa Henry wakati wa mafunzo kwa timu ya uwezeshaji na uratibu wa kamati za ukimwi ambapo amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwezesha Halmashauri na kata kuboresha mifumo ya huduma za afya na ustawi wa jamii kupunguza maambukizi na madhara ya virusi vya UKIMWI kwa makundi maalum, kujengea uwezo wa uratibu, ushawishi na utetezi kwa masuala ya UKIMWI kwa jamii na kuwezesha masuala ya usimamizi shirikishi wa kamati za kudhibiti UKIMWI za kata ziweze kutekeleza majukumu yake.
Licha ya kubainisha malengo ya mafunzo hayo Mkurugenzi wa JSI Kanda ya Pwani Pamela Msei amesema kuwa kamati hizo zinao wajibu na majukumu ya kuhakikisha kamati za VVU na UKIMWI zinaundwa na kufanya kazi kwa kila ngazi kwa kufuata miongozo, kuhakikisha tathmini ya hali halisi ya VVU na UKIMWI katika Halmashauri inafanyika na kuweka mikakati ya utekelezaji kila mwaka, kuhakikisha mipango yote ya UKIMWI na wadau wanaotekeleza katika Halmashauri husika vinaingizwa kwenye mpango mkakati wa Halmashauri na mkoa kuondoa urudufu wa juhudi za rasilimali sambamba na kuhakikisha sheria ndogo, mkakati wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI, sheria, miongozo na matokeo ya tafiti mbalimbali ya masuala ya UKIMWI yanawafikia wadau na wananchi kwa ujumla.
Naye Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Kilosa Emeresiana Temu amesema kuwa programu ya uimarishaji mifumo ya afya ya jamii na ustawi wa jamii kwa kamati za ukimwi ngazi ya kata yanaendelea chini ya halmashauri yakifadhiliwa na shirika la jsi research katika kata tano ambazo ni Magomeni, Kasiki, Mbumi, Mkwatani na Mabwerebwere lengo ikiwa ni kuhakikisha kamati hizo zinafanya kazi na kuwasilisha taarifa zao kwa mratibu kila robo ya mwaka ambapo kamati hizo zitafanya kazi ya kujua hali ya maambukizi ya VVU/UKIMWI kupitia kata zao na kutengeneza mikakati ya namna ya kutokomeza kuwepo kwa maambukizi mapya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa