Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambaye pia ni diwani wa kata ya Mvumi Mh.Hassan Mkopi amezitaka kamati mbalimbali zinazosimamia miradi katika ngazi ya kata na vijiji kutambua kuwa fedha zinazopelekwa katika miradi zinawahusu wao hususani katika taratibu zote za ujenzi, manunuzi, mapokezi na matumizi ya vifaa mbalimbali kwani miradi inayofanyika katika maeneo yao ni kwa faida yao na vizazi vyao.
Mkopi amesema hayo Aprili 23 mwaka huu alipokuwa ameambatana na kamati ya uchumi, uongozi na mipango walipofanya ziara ya kutembelea kituo cha mafunzo ya kilimo na mifugo(waki) kilichopo katika kata ya Ulaya ambapo amesema kamati zina wajibu wa kujua mlolongo mzima wa ujenzi, manunuzi na taratibu nyinginezo badala ya kuwaachia wataalam toka wilayani wafanye kila kitu kwani kabla ya kuanza kwa miradi hiyo wanapewa maelekezo namna ya utendaji ili kufanyika kwa miradi hiyo.
Mkopi amesema kuwa wilaya ya kilosa ni kubwa hivyo ni vema kuthamini kila wanachokipokea kwa kuhakikisha fedha yoyote inayoelekezwa katika miradi wanafahamu vizuri matumizi yake ikiwemo taratibu za upatikanaji wa mafundi, upatikanaji wa wazabuni, manunuzi ya vifaa, mapokezi na hukakikisha fedha inatumika kama inavyostahiki na kutoa miradi inayolingana na thamani ya fedha iliyotolewa na kwamba uwepo wa BOQ ni jambo moja na utekelezaji wa BOQ ni jambo jingine hivyo kila wanapopokea fedha ni vema kila mwanakamati akawa na uelewa na kumbukumbu ya namna fedha hizo zinavyotumika.
Naye diwani wa viti maalum Mh Anna Sanga amesema ni vema wanakamati hao wakajikita katika kutumia kila fursa inayojitokeza kwa kujiletea maendeleo kwani wilaya ya Kilosa ni kubwa na ina hivyo sio kila mara itaangaliwa kata moja bali kata zote na inapotokea fedha imepelekwa katika kata yao ni vema wakahakikisha fedha hiyo inatumika vizuri na kwa viwango vinavyostahiki.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa