Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amewataka Watumishi wa Umma kiujumla wilayani Kilosa kupenda kazi zao na kuwajibika inavyostahili na kuwa chachu ya maendeleo kwa kutunza rasilimali mbalimbali katika ofisi zao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi huyo Septemba 11 mwaka huu wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa Idara ya Ujenzi mara baada ya kutembelea karakana ya ujenzi na maeneo yote ya ofisi za ujenzi ambapo amesema kuwa mtumishi yoyote anapaswa kuipenda kazi yake kwani ndiyo inayomuwezesha kujimudu kimaisha na kupata maendeleo yake binafsi na Halmashauri kwa ujumla.
Licha ya kutoa rai hiyo Mwambambale amemwagiza Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Wilaya kuandaa barua itakayoenda chuo cha ufundi VETA ili waweze kutembelea eneo la ujenzi na kutoa ushauri namna ya kufufua karakana ya useremala itakayotumika kama chanzo cha mapato kwa kutengeneza samani mbalimbali za Halmashauri na za kuuza, huku akiagiza ufanyike mchakato wa kupata mashine ya umeme ya kufyatua matofali ambayo itasaidia kufyatua tofali zenye ubora zitakazotumika katika majengo ya Halmashauri lakini pia kuyauza kwa wadau mbalimbali ili kuiongezea Halmashauri mapato.
Aidha ameitaka idara hiyo kuainisha mapungufu yote yaliyopo katika magari ili kubaini marekebisho/ukarabati wake pamoja na gharama ili yafanyiwe matengenezo kwa gharama nafuu ili baada ya matengenezo hayo yaweze kujiendesha, huku kwa upande wa wahandisi na mafundi ujenzi wakitakiwa kuongeza kiwango cha usimamizi katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya Halmashauri kuanzia hatua za awali za ufyatuaji matofali hadi jengo kamili kwa kuzingatia ubora unaokubalika kwa gharama nafuu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa