Kuna changamoto mbalimbali katika mnyororo wa thamani ya mazao ikiwemo upotevu wa mazao ambapo inakadiriwa kati 30% hadi 40% ya mazao ya chakula hupotea baada ya kuvuna kila mwaka kutokana na teknolojia duni za kuhifadhi mazao baada ya kuvuna, uelewa mdogo wa wadau katika kukabiliana na upotevu wa mazao pamoja na uhaba wa miundombinu ya masoko.
Hayo yamebainishwa Machi 10 mwaka huu na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Francis Kaunda katika mafunzo ya mkakati wa taifa wa usimamaizi wa mazao baada ya kuvuna ambapo amesema upotevu wa mazao ni tishio kubwa kwa usalama wa chakula kwa nchi yoyote duniani, kwani nchi isipojitosheleza kwa chakula husababisha wananchi wake kuwa na afya duni, dhaifu, wasioweza kufanya shughuli za uzalishaji, wasioweza kujishughulisha katika shughuli za kijamii ikiwemo kuandaa watoto katika masomo kwa ajili ya maisha yao ya baadae na kwa maendeleo ya nchi kiujumla.
Kaunda amesema kuwa upotevu wa mazao huhatarisha usalama wa nchi kwani inakuwa vigumu kwa kiongozi kutawala na kuongoza taifa la watu wenye njaa, pamoja na hayo upotevu wa mazao baada ya kuvuna hupoteza mapato kwa wahusika kwa katika mnyororo wa thamani na kuwakatisha tamaa kuendelea na shughuli za uzalishaji ambapo mkulima kipato hupungua halkadhalika mapato ya ndani kwa Halmashauri yatapungua ambayo husaidia katika kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo mazao hayo yakiwa katika usimamizi stahiki yatakuwa katika kiwango kinachoridhisha.
Pamoja na hayo amesema ili kukabiliana na changamoto za upotevu wa mazao Serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa kupunguza upotevu wa mazao unaolenga kukabiliana na upotevu wa mazao baada ya kuvuna ambapo katika mkakati huo maeneo kwa kushughulikia maeneo tisa ili kuimarisha usalama wa chakula na lishe ambapo kila wilaya litaundwa jukwaa la wadau wa masuala ya usimamizi wa mazao baada ya kuvuna ili kujadili namna endelevu ya usimamizi wa mazao baada ya kuvunwa.
BAADHI YA WADAU WAKIWA KATIKA MAFUNZO HAYO.
Maeneo yanayopaswa kushughulikiwa ni uelewa mdogo kuhusu upotevu wa mazao baada ya kuvuna ikiwa ni pamoja na vyanzo vyake,athari zake na ufumbuzi wake kwa wahusika katika mnyororo wa thamani, pili ni upatikanaji mdogo wa teknolojia fanisi na za gharama nafuu za usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, tatu mifumo duni na isiyotosheleza ya kimasoko na miundombinu ya mazao ya chakula, nne tafiti chahche na ubunifu mdogo katika masuala ya usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, tano ni usimamizi duni wa kanuni na miongozo ua usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, sita uwezo mdogo wa kitaasisi, uratibu usiotosheleza na ushiriki mdogo wa wadau wengine katika usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, saba uwezo mdogo wa kutambua na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi juu ya usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, nane uwekezaji mdogo wa kifedha kwenye shughuli za usimamizi wa mazao baada ya kuvuna na mwisho ni ukosefu wa twakwimu na taarifa sahihi za upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa