Katika kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi hususani wa kike na kusababisha kutofikia malengo yao kielimu Halmashauri ya wilaya ya Kilosa imeazimia kujenga shule ya sekondari ya bweni kwaajili ya watoto wa kike kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, michango ya wananchi na kwa wadau wa maendeleo.
Hayo yamebainishwa Septemba 17 mwaka huu na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Asajile Mwambambale wakati wa kikao maalum kilichoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama, timu ya menejimenti, maafisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji na ambapo Mgeni rasmi wa kikao hicho akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh Adam Mgoyi.
Mwambambale amesema kuwa katika safari ya kutafuta elimu watoto wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule, kuozeshwa, kurubuniwa na wanaume hali ambayo imekuwa ikiwarudisha nyuma katika kutimiza malengo yao na kusema kuwa ndiyo maana wamekuja na mpango huo wa kujenga shule ya bweni ili ikawe mkombozi wa wanafunzi wa kike.
Mwambambale amesema mpango huo unatarajiwa kutekelezwa haraka iwezekanavyo huku ikitarajiwa ifikapo mwaka 2021 wanafunzi wa kidato cha kwanza waanze kusoma katika shule hiyo na kwamba tayari maandalizi ya awali ya ujenzi wa shule hiyo yamekwishaanza ambayo mpaka kukamilika kwake itatumia shilingi milioni 861 na huku zoezi la ufyatuaji tofali likianza Septemba 18 mwaka huu.
Aidha amesema shule hiyo itajengwa katika eneo la Kondoa katika kata ya Mabwerebwere ambapo kuna eneo la hekari 16 na tayari tripu 60 za mchanga na saruji mifuko 1,800 vimeshapelekwa katika eneo la mradi tayari kwa kazi ambapo amewataka viongozi hao kuweka nguvu ya pamoja katika kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kuchangia ujenzi huo kwaajili ya kumkomboa mtoto wa kike wa Wilaya ya Kilosa.
Nao viongozi hao wamepokea suala hilo kwa mikono miwili na kuupongeza uongozi kwa maono mazuri waliyonayo katika sekta ya elimu huku wakiahidi wao binafsi kuwa mstari wa mbele kwa kuchangia na kuhamasisha wananchi katika kuchangia ili ujenzi wa shule hiyo uweze kukamilika kama ilivyopangwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa