Rai imetolewa kwa Watendaji wa kata, walimu wa wakuu pamoja na waratibu elimu kati kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi wa boost ambao unatekelezwa nchi nzima ambapo utanufaisha jamii katika suala zima la elimu. na kipaumbele kikiwa elimu ya msingi kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba amesema upatikanaji wa fedha za mradi huo utategemea zaidi matokeo ya utekelezaji kwani ndio yatakayopelekea wilaya kupata fedha zaidi na kwamba Wilaya ya Kilosa inalo jukumu kubwa sana la ujenzi wa madarasa hivyo mradi huo ni fursa na unapaswa kusimamiwa ipasavyo kwa kuhakikisha watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza wanaandikishwa ipaswavyo.
Kisena amesema kuwa yapo maeneo nane ambayo yatasaidia utekelezaji wa mradi wa boost ikiwemo Mpango wa kuendelezwa miundombinu ya shule inayozingatia mahitaji kwa elimu ya awali na msingi, Mpango wa shule za msingi salama,kuongeza asilimia ya uwiano wa uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, Utekelezaji wa njia bora na matumizi ya vifaa stahiki vya kujifundishia na kujifunzia katika madarasa ya elimu ya awali, Utekelezaji wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini(MEWAKA), Idadi ya shule za msingi na vituo vya walimu zinazotekeleza mtaala wa TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia vinavyowezeshwa kupitia mfumo wa usimamizi wa ujifunzaji, Utengaji wa bajeti kwa ajili ya kuwezesha shughuli muhimu za programu na kuhakikisha kuwa kiwango cha bajeti kinadumishwa na kuongezwa pamoja na suala zima la Halmashauri zinazokidhi vigezo vya utawala bora katika elimu.
Mradi wa boost unakwenda kujenga shule mpya, kukarabati shule za zamani na kujenga nyumba za walimu hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha maeneo yanayotarajiwa kujengwa lazima yazingatie maeneo nane lakini pia suala zima la uandikishwaji wanafunzi wa awali na darasa la kwanza liwe ni ajenda kwani mradi unategemea kujenga madarasa ya awali ambayo yanapaswa kuwa rafiki kwa mtoto ili apende kwenda shule.
Kisena amesema kuwa malengo ya program ya boost ni kuboresha upatikanaji fursa sawa katika ujifunzaji bora wa elimu ya awali na msingi Tanzania Bara na ni sehemu ya Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu awamu ya pili(EPforR II) na inachangia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa sekta ya elimu wa miaka mitano 2021/22 hadi 2025/26.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi na Awali Wilaya Zakia Fandey amesema ili kufanikisha mradi huo kila mmoja anao wajibu wa kushiriki kikamilifu kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa Wilaya kupata vyumba vya madarasa, nyumba za walimu hivyo unahitaji ushiriki wa kila mmoja ili kuufanikisha kwa maslahi mapana ya sekta elimu kwa Wilaya ya Kilosa
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa