Katika kuhakikisha sekta ya mifugo na uvuvi inasonga mbele kwa kasi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 28 .1 kwa ajili ya mapinduzi katika sekta hiyo ili kuleta mabadiliko kwa kuwa na ufugaji wenye tija nchini.
Dkt. Ashatu ameyasema hayo 3 Januari , 2025 wakati akizindua mashamba ya malisho ya mifugo katika Vijiji vya Mandela na Mbwade Wilayani kilosa ambapo amesema kuwa mkoa wa morogoro unakwenda kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya ufugaji wa kisasa utakaopelekea kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima pia kuongeza masoko nje ya nchi na kuinua uchumi kwa wafugaji.
Dkt. Ashatu ameongeza kuwa wafugaji wote wanatakiwa kuwa na maeneo ya malisho sambamba na visima vya maji, kuwapatia chanjo mifugo yao pamoja na utambuzi wa mifugo ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kufanya mipango ya maendeleo.
Sambamba na hayo Waziri Ashatu ameeleza kuwa serikali itafanya maboresho kwa kutoa vitendea kazi ambapo maafisa ugani watanunuliwa pikipiki mia saba (700 ) na vishkwambi elfu nne mia tano (4500) ambapo kupitia vitendea kazi hivyo vitawarahisishia maafisa ugani hao kuweza kufanya kazi kwa weredi na kuondokana na changamoto ya usafiri na utunzaji wa takwimu kidigitali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka Maafisa Watendaji wa kata na Vijiji kuacha kufanya tathmini ya ulishwaji wa mazao isiyo ya kweli na kupelekea kumuonea mkulima na badala yake wafanye tathmini ya kweli ili mkulima alipwe kulingana na kile alichopoteza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu asilimia kubwa wilaya ya kilosa imepunguza vifo vinavyotokana na migogoro ya Wakulima na wafugaji kutokana na njia mbalimbali zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Pia chifu Matayane Simanga ambaye ni chifu wa wamasai ameshukuru kwa ujio wa Mhe. Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyoongelewa na kusema kuwa wataendelea kuhamasisha jamii za wafugaji kufuata njia za ufugaji wa kisasa ili kuepukana na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa