Katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika za Zanzibar Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh Shaka H. Shaka ametoa rai kwa wanakilosa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Rai hiyo imetolewa Aprili 26 mwaka huu wakati wa zoezi la upandaji miti katika eneo la mto Mkondoa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo amesema kuwa Serikali imekuwa ikikabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kupanda miti nyakati zote na kwamba kwa mwaka 2022/23 Wilaya ya Kilosa inapaswa kupanda miti ipatayo 1,500,000.
Licha ya mabadiliko ya tabia nchi Mh. Shaka amesema kumekuwa na tabia ya ukataji mito na kutothamini misitu jambo ambalo si sahihi, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kutunza mazingira kwa kufanya jitihada za upandaji miti kuwa zoezi endelevu na kwamba hadi sasa wilaya imefanikiwa kupanda miti 789,000, pia amewataka viongozi wa kata na vijiji kujiwekea malengo ya upandaji miti kuanzia ngazi ya kata kupanda miti takribani 500 kwa mwezi jambo litakalosaidia kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali huku akizitaka taasisi zilizopo Kilosa kushiriki katika kampeni ya upandaji miti sambamba na utoaji elimu wa namna ya utunzaji miti yote inayopandwa na ambayo imeshapandwa.
Pamoja na hayo amewataka wanakilosa kufahamu kuwa Muungano umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mwingiliano wa kimahusiano baina ya Tanzania bara na visiwani, uwepo wa amani, uendelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, kufunguka kwa nyanja za kiuchumi na kwamba watanzania tunayo kazi ya ya kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama tunu ya Taifa ili kulifanya Taifa kuwa lenye umoja na mshikamano.
Kwa upande wake Katibu Tawala Yohana Kasitila amesema upandaji miti umefanyika katika mto Mkondo kwa lengo la kuendeleza utunzaji wa mto huop ili kuondoa adha ya mafuriko kwani mara nyingi mto huo umekuwa ukikumbwa na mafuriko na kwamba kampeni ya upandaji miti itakuwa endelevu katika mito mingine iliyopo wilayani Kilosa.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa upandaji miti Afisa Maliasili Sadala Ally amesema zoezi la upandaji miti kwa Wilaya ya Kilosa ni endelevu ambalo linashirikisha wadau mbalimbali ambapo ili kukabiliana na changamoto za uchomaji moto, kung’olewa kwa miti hovyo, miti kuliwa na mifugo wakati wa kiangazi halmashauri imejipanga kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa jamii, uanzishaji wa klabu za mazingira mashuleni, kuunda, kusimamia na kuboresha kamati za maliasili, kutoa elimu ya utunzaji vyanzo vya maji, kuhamasisha Serikali za vijiji kusimamia miti iliyopandwa na kukuendelea kutenga bajeti ili kuwezesha shughuli za upandaji miti.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa