Katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara, Halmashauri ya wilaya ya kilosa imeonesha mfano bora wa kushirikiana kwa pamoja katika shughuli za kijamii kupitia zoezi la usafi likiongozwa na Katibu tawala Bi. Salome Mkinga ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, la kuzitaka Taasisi za umma na Halmashauri zote kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii.
Akiwaongoza wananchi kushiriki zoezi hilo lililofanyika katika Mamlaka ya Mji Mdogo mikumi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Bi. Salome Mkinga amesema utamaduni wa kufanya usafi usiishie hapo bali uwe endelevu kwa ajili ya kudumisha suala zima la afya lakini pia ustawi wa jamii kwa ujumla.
Bi. Salome ameongeza kuwa kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya wafanyabiara na wananchi kutupa taka maeneo yasiyo rasmi ikiwemo kwenye mitalo hali hiyo hupelekea mifereji kuziba ambapo baada ya mvua kunyesha magonjwa ya milipuko hutokea katika maeneo yao.
“Mikumi ni kitovu kizuri zaidi cha Biashara kuna biashara gani ambayo ni nzuri inafanyika sehemu ambayo ni chafu? kumvutia mteja sehemu inatakiwa kuwa safi” Alisema Bi. Salome.
Sambamba na hayo amesema kuwa hivi karibuni kunatarajiwa kupatikana mzabuni atakayekuwa anahusika na kukusanya taka hivyo amewaomba wananchi kumpa ushirikiano wa kutosha pale atakapohitaji ushirikiano huo kutoka kwao ili kusaidia uimarishaji wa usafi katika maeneo mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa