Katika kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeadhimisha siku hiyo kwa kupanda Miti 158 katika shule ya Msingi Lamlilo iliyopo kata ya Magomeni.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Aprili 26, 2025 Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa Ndg. Shadrack E. Sadatale amesema ni muhimu jamii ikapewa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira hususani upandaji wa miti katika maeneo yao ambapo mazingira hayo yatasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Nchi inapofanya mabadiliko usipochukua hatua kama hizi baadae Taifa linakuwa kwenye majanga makubwa sana”. Alisema Sadatale
Pia Sadatale ameongeza kuwa zoezi hilo likawe endelevu katika jamii na ikiwa mazingira yatatuzwa vizuri nayo pia yataitunza jamii ambapo amesema zipo faida nyingi sana za utunzaji wa mazingira hivyo amewasihi wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira yao na endapo kutatokea na uharibifu wa mazingira wa aina yeyote watoe taarifa kwa vyombo au mamlaka husika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Amani Mkandarasi amesema siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni siku maalumu sana katika taifa la Tanzania ambapo amewashuruku wananchi wote kujitokeza kuungana kwa pamoja katika zoezi la upandaji miti.
“Muungano maana yake ni umoja tuko hapa katika kuimarisha umoja wa taifa letu la Tanzania” . Alisema Mkandarasi
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa