Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na wakuu wa idara na Wakuu wa taasisi mbalimbali wamezindua ujenziwa kituo kidogo cha Polisi katika kata ya Tindiga ikiwa ni katika harakati za kuleta amani na utulivu .
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika hivi karibuni Mh Majid amesema kuwa ujenzi huo wa kituo cha polisi ni katika kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa hivi karibuni la kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji lakini pia kutaka wafugaji wajengewe uwezo ili kufanya ufugaji wa kisasa.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema Wilaya imejipanga kutekeleza agizo hilo kwa kuanzisha kituo hicho cha polisi ili kuimarisha amani na utulivu katika eneo hilo na maeneo mengine kwa ujumla.
Pamoja na hayo amewaomba wananchi wa Kata ya Tindiga kuunga Mkono Mh Rais kwa kudumisha amani kwa kuacha kutumia nguvu au kujichukulia sheria mkononi badala yake kuripoti katika sehemu husika endapo kutatokea uvunjifu wa amani wa aina yeyote.
Aidha Mh Majid amewaasa wananchi wa kata hiyo ya Tindiga kuwapa ushirikiano maaskari watakaopangiwa kufanya kazi katika kituo hicho na kuishi nao kama vijana wao ili kwa pamoja waweze kudumisha amani.
Kituo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu na kwa sasa kipo katika hatua ya msingi na kinajengwa kwa michango ya wadau ikiwemo ofisi ya Mkurugenzi na Taasisi mbalimbali zilizopo wilayani hapa.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa Kisena Mabuba aliwataka wanachi wa Tindiga kuheshimiana na kuishi kwa amani na utulivu huku akiagiza viongozi wa vijiji kutofumbia macho mtu yeyote anayeunja amani awe mkulima au mfugaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa