Licha ya kutoa pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameitaka Halmashauri kuendelea kulinda mafanikio waliyoyapata ya kupata hati inayoridhisha kwa kuhakikisha inaondoa makando kando yote yanayosababisha kuwa na hati isiyoridhisha ambapo kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2015/16, 2016/17, 2017/18 na 2018/19 Kilosa imekuwa ikipata hati inayoridhisha.
Sanare ametoa rai hiyo Mei 6 mwaka huu wakati wa baraza maalum la madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa na majibu ya hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali za mwaka wa fedha 2018/19 ambapo ametaika Halmashauri kuendelea na mwenendo wa utendaji kazi mzuri kwa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea hususani kwa watendaji na wasimamizi wa shughuli za kimaendeleo ndani ya Halmashauri.
Sanare amesema mkaguzi katika taarifa yake ameonyesha kumekuwa na udhaifu katika baadhi ya maeneo ikiwemo kutozingatiwa kwa baadhi maelekezo ya serikali ambayo yamesababisha hoja ambazo hazijafungwa hivyo ametaka hoja zote ambazo hazijafungwa ziweze kushughulikiwa ipasavyo na hoja zote zinazojitokeza kutekelezwa ipasavyo ili kuepusha uwepo wa hoja huku akilitaka baraza la madiwani kuchukua hatua kwa watumishi wote waliosababisha kuwepo kwa hoja.
Pamoja na hayo amewataka madiwani kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuhamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo na kuhakikisha miradi inayoanzishwa inakamilishwa ikiwemo kuwachukulia hatua watumishi wanaosababisha ubadhilifu wa fedha katika miradi hiyo.
Aidha ametaka kufanyika usimamizi wa kutosha katika utendaji kazi wa serikali ili kudhibiti uwepo wa hoja kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za utendaji kazi serikalini, huku akitaka kuwepo kwa uadilifu katika matumizi ya fedha za Serikali ambapo pia ametaka wakuu wa idara wanaokaimu nafasi za ukuu wa idara kwa muda mrefu kufanyika mchakato wa kuhakikisha nafasi hizo zinakuwa na wakuu wa idara kamili badala ya makaimu hao kukaa katika nafasi hizo kwa muda mrefu.
Akizungumzia upande wa mapato amesema kiasi cha fedha kilichokusanywa ni nusu ya malengo yaliyokusudiwa hivyo ametaka kufanyika kwa tafiti na ufuatiliaji wa makusanyo katika maeneo yote kwani ili shughuli za maendeleo zifanikiwe lazima kuwe na makusanyo ya aina mbalimbali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Akihitimisha maagizo na maelekezo yake Sanare ametaka kuundwa kwa timu maalumu ya kufanya ukaguzi kwa wasambazaji wa sukari na kuhakikisha sukari inakuwepo maeneo yote na inauzwa kwa bei elekezi ya shilingi 2700 kwa kilo kwa kila duka na kwa yoyoyte atakayebainika kuuza sukari kwa bei ya juu hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake ikiwemo wale wauzaji wanaoficha sukari na kusababisha uhaba wa sukari.
Akitoa taarifa mkaguzi wa hesabu za Serikali Peter Mwambwanga amesema utaratibu wa ukaguzi wa matumizi ya fedha za Serikali unalenga kuangalia endapo matumizi ya fedha za Serikali kama yamefuata taratibu stahiki ambapo ukaguzi ulifanyika katika mamlaka za serikali 185 zilizokaguliwa halmashuri 176 zilifanya vizuri huku Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ni mojawapo ya Halmashauri zilizofanya vizuri na kwamba katika Mkoa wa Morogoro halmashauri zote 9 zimefanya vizuri na kupata hati inayoridhisha.
Mwambwanga amesema kamati ya bunge ya hesabu za Serikali za mitaa ilitoa maagizo manne kwa ajili ya kuiboresha Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambapo maagizo matatu yameshatekelezwa huku moja likiwa katika ngazi ya utekelezaji na kwamba ikifanyika tahmini toka mwaka 2015/16 hadi 2018/19 imekuwa ikipata hati inayoridhisha na kwamba katika maoni 37 yaliyotolewa kwa halmashuri maoni 30 yameshafanyiwa kazi kikamifu na kubakiza maoni 7 ambayo ni sawa na asilimia 81 ya utekelezaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amesema kuwa maagizo na maelekezo yaliyotolewa kama halmashauri wameyachukua na kuyafanyia kazi huku akimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara zake ambazo zimekuwa zikichagiza na kuboresha utendaji kazi na usimamizi ndani ya wilaya lengo likiwa ni utoaji wa huduma kwa jamii ambao ndo msingi ndio dhamira ya Serikali ya awamu ya tano chini Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Mwambambale amesema kama halmashuri wanajitahidi kuzingatia maelekezo ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali na ndio maana kumekuwa kunakupungua kwa hoja hizo na anawashukuru waheshimiwa madiwani na watendaji kwa ushirikiano wao na kwamba kama halmashuri wanajipanga kuhakikisha hoja hizo zinapungua zaidi na ikiwezekana halmashuri kutokuwa na hoja kabisa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa