Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeendelea kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 ambao unakwenda sambamba na falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya hapa kazi tu lengo ikiwa ifikapo mwaka 2025 kuwe na Taifa lenye maisha bora kwa kila mtanzania.
Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila amebainisha hayo Machi 3 mwaka huu alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015- 2020 kwa kipindi cha mwezi Julai 2018 hadi Disemba 2019 kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ambapo amesema taarifa hiyo imetekeleza kwa vitendo ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambayo inatoa dira ya utekelezaji Sera za Serikali kwa kuzingatia masuala ya msingi.
Akieleza masuala hayo Kasitila amesema mojawapo ya mambo hayo ni kujenga uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea kwa kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuwawezesha wananchi kiuchumi ili waweze kumiliki na kuendesha uchumi na kipato kwa wananchi pamoja na kujenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogo kwa lengo la kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi hasa vijana.
Kasitila amesema kuwa katika utekelezaji huo Halmashauri imetekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa utoaji asilimia kumi ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa 2018/2019 shilingi 221,114,629.00 kwa vikundi 51, mwaka wa fedha 2019/2020 hadi kufikia Disemba 2019 jumla ya shilingi 180,099,842.08 kwa vikundi 26 ambapo pia Halmashauri imejiwekea mkakati kuhakikisha kwa kila mapato ya ndani yanayopatikana asilimia 10 lazima itengwe na kupelekwa kwa vikundi hivyo.
Aidha upande wa sekta ya afya Halmashuri imekamilisha ujenzi wa kituo cha afya Mikumi ambapo pia kimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje ambapo pia amesema ujenzi katika vituo vya afya Malolo na Mvumi unaendelea wakati huo katika kuhakikisha uzazi salama wa mama mjamzito na mtoto unakuwepo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeanza kutoa huduma katika wodi mpya ya wazazi kwa kiwango kinachoridhisha tofauti na jengo la awali ambalo miundombinu yake ilikuwa hairidhishi.
Kwa upande wa sekta ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia Serikali imeendelea kuleta pesa ili kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu mipya , kukarabati na kufanya umaliziaji wa miundombinu iliyoanzishwa na wananchi katika maeneo mbalimbali huku upande wa sekta ya uchumi (kilimo na umwagiliaji) kwa kuhakikisha mnyororo wa thamani ya mazao kwa wakulima unaongezeka ambapo Serikali imetoa shilingi 971,311,119.00 kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao Mvumi.
Licha ya hayo katika sekta ya maji Halmashauri imetoa shilingi 70,000,000.00 kutoka katika mapato yake ya ndani ikiwa ni utekkelzaji wa agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu katika eneo la Ruaha kwenda kwenye akaunti ya RUWASA ambapo hadi sasa mradi umetekelezwa kwa 80%.
Kasitila amesema mchango wa Halmashauri katika utekelezaji shughuli za maendeleo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya shilingi 1,097,454,134.93 zilielekezwa katika shughuli za maendeleo huku Julai hadi Disemba shilingi 632,426,640.97 zikielekezwa katika shughuli za maendeleo
Katika utekelezaji huo Kasitila amesema zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji iliyosababisha uharibifu wa mali, binadamu, mifugo na mazao, baadhi ya skimu za umwagiliaji kushindwa kutumika kikamilifu kipindi cha kiangazi kutokana na mifugo ya wafugaji kuvamia mashamba ili kufata malisho na maji, athari za mafuriko katika kata mbalimbali na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya kitaifa ya Reli ya Kati na barabara kuu hususani barabra za Mikumi-Kilosa-Dumila, Kilosa-Melela-Morogoro na Morogoro-Dumila-Dodoma pamoja na uhaba wa watumishi katika kada mbalimbali hususan sekta ya afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa