Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyombo vya usafiri Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ilifanikiwa kununua magari mawili kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ili kupunguza adha ya changamoto hiyo ingawa upungufu bado ni mkubwa.
Hayo yamebainishwa Desemba 19, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba Mkurugenzi wakati akitoa taarifa ya Halmashauri mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Manenimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya siku moja ambapo alizungumza na watumishi wa Umma katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Ilonga.
Mabuba amesema kuwa licha ya ununuzi wa magari hayo pia amesema Halmashauri imetenga bajeti ya kununua magari mengine mawili, na kwamba katika bajeti ya mwaka huu imepanga kununua pikipiki 40 kwaajili ya watendaji wa kata ili ziwasaidie katika utendaji kazi kwani kata nyingine ziko umbali wa zaidi ya kilometa 300 mpaka kufika makao makuu ya Wilaya.
Sambamba na hayo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa inayoendelea katika kupunguza malalamiko na kero za watumishi ambapo amesema Halmashauri kwa mwaka huu wa fedha imepokea watumishi wapya 198 katika kada mbalimbali kwa kiasi kikubwa watasaidia kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha amesema kuwa Halmashauri inaendelea kutatua kero za watumishi zilizo ndani ya uwezo na zile ambazo ziko nje ya uwezo zinapelekwa mahala panapohusika ili ziweze kutatuliwa huku akisema katika mwaka wa fedha ulioisha takribani watumishi 800 wa kada mbalimbali wameweza kupandishwa madaraja na vyeo pia kulipwa malimbikizo mbalimbali ya madeni ikiwa ni hatua kubwa iliyofanywa na Serikali.
Akieleza mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu(TASAF) Mratibu wa TASAF Wilaya Dedan Maube amesema wanafunzi 10,705 kutoka katika kaya za walengwa wananufaika na ruzuku ya masharti ya elimu hivyo kupelekea kuinua mahudhurio yao hadi kufikia zaidi ya asilimia 90 huku watoto 1988 kutoka katika kaya za walengwa wananufaika na ruzuku ya masharti ya afya lakini pia Mpango umeweza kuvifikia vijiji vyote 138 na mitaa 18 ya Wilaya ya Kilosa ambapo kaya 10572 zinanufaika na mpango huku miradi ya Visima 14 ikitekelezwa na mtandao wa maji bomba katika vijiji vya Makwambe, Manzese, Madudumizi, Nyangala, Ilakala na Rudewa Mbuyuni kupitia Miradi ya ajira za muda kuwasaidia akina Mama na watoto ambapo wameupukana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na pia kuepukana na magonjwa yanayohusiana na kunywa maji yasiyo salama ya mito.
Maube amesema ujenzi wa vivuko na mitaro ya kutiririsha maji umesaidia kuondoa mafuriko kwenye makazi ya wananchi katika vijiji vya Rose, Behewa, Kiyangayanga, Mbwamaji, Ruaha, Tundu na Mtumbatu lakini pia utekelezaji wa miradi ya Miti umewezesha uboreshaji wa mazingira yalioharibiwa na shughuli za kibinadamu na imesaidia kurudisha uoto wa asili ulioharibiwa katika maeneo husika na watoto wa kike 3140 kutoka familia za walengwa wenye umri wa miaka 11 walipatiwa taulo za kike za kisasa na vifaa vya usafi na baadhi ya Kaya zimeboresha makazi, kujishughulisha na kilimo , kufuga mifugo midogo midogo kama kuku, bata, kondoo na mbuzi, kadhalika kuanza biashara ndogondogo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa