Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2022 Bw. Sahili Gereruma ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Kilosa pamoja na wananchi kiujumla kwa kutekeleza ipasavyo miradi iliyotembelewa na mbio za Mwenge wa Uhuru na yote kukubalika ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 25, 2022 wakati mwenge ukikimbizwa Wilayani Kilosa na kutembelea miradi mitano iliyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.4 ambapo umeweka jiwe la msingi Kituo cha Afya Nhembo kata ya Mabula, na Mradi wa maji Rudewa, pia umezindua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Mlingotini, huku ukitembelea na kuona uendeshaji wa shughuli za vijana katika kikundi cha Tunaweza sanaa pamoja na kushuhudia na kufungua mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja ya walimu shule ya sekondari Dumila.
Aidha Bw. Geraruma amewaagiza kumaliziwa kwa miradi ambayo inaendelea ikiwemo kuzingatia taratibu zote za usimamizi wa miradi, ushiriki wa wataalam katika miradi ili kutoa ushauri wa kitaalam wakati wa utekelezaji wa miradi, ukamilishaji wa miradi kwa wakati, kujengea uzio vituo vyote vya kuchota maji huku akiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuvuta maji katika nyumba zao ili kutimiza dhana halisi ya kumtua mama ndoo kichwani sambamba na kushiriki kikamilifu sensa ya watu na makazi hususani kwa wale ambao bado hawajahesabiwa kwani zoezi la sensa bado linaendelea.
Akitoa Ujumbe wa Mwenge mmoja wa wakimbiza Mwenge kitaifa Zabida A. Rashid amesema ujumbe wa mbio za mwenge umezingatia hoja na vipaumbele sita ambapo unasisitiza juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kaulimbiu ya Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo, Shiriki Kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa huku ukiendelea kuhamasisha jamii kuhusu kuzingatia lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi ameshukuru Mh. Samia Suluhu kwa fedha za miradi inayoendelea wilayani Kilosa huku akiwasihi kutokata miti hovyoili kutunza vyanzo vya maji.
Aidha Mwenge wa Uhuru umekamilisha mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa salama na kukabidhiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa