Katika kuhakikisha watoto wanasoma vizuri wawapo shuleni kwa shule za msingi na sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imejiwekea mikakati mbalimbali ya upatikanaji wa chakula shuleni ikiwemo matumizi ya mashamba yanayomilikiwa na shule kwa ajili ya kilimo.
Mikakati mbalimbali imewekwa katikati ya wiki wakati wa kikao cha robo ya kwanza ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Shaka H. Shaka ambapo ametaka mikakati iliyowekwa kusimamiwa na kutekelezwa ili watoto wote waweze kupata chakula shuleni.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni pamoja kwenye kikao hicho ni matumizi ya mashamba yanayomilikiwa na shule kutumika kwa ajili ya kilimo ili mazao yatakayopatikana yaweze kutumika kwa ajili ya chakula.
Mikakati mingine ni kuwepo kwa sheria ndogo itakayowashirikisha wazazi na walezi kushiriki katika kuhakikisha watoto wote wanapata chakula wawapo shuleni, kuendelea kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa watoto kupata chakula sambamba na walimu kuendelea kusimamia na kuhamasisha wazazi na jamii kushiriki zoezi la upatikanaji chakula shuleni.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Wilaya, wakuu wa idara mtambuka pamoja na watendaji wa kata zote ambapo wamesisitizwa kuendelea kutumia siku ya lishe katika maeneo yao kwa kutoa elimu ya umuhimu wa upatikana wa chakula shuleni.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa