Halmashauri ya wilaya ya Kilosa imeendelea kutekeleza shughuli za maendeleo jambo ambalo limeleta tija katika jamii ambapo,imeweza kumudu kupata hati safi kwa miaka mitano mfululizo lakini pia imeweza kutekeleza shughuli za miradi kwa mapato yake ya ndani.
Akifungua kikao cha baraza la madiwani makamu mwenyekiti ambaye alikuwa Mwenyekiti katika kikao cha baraza la madiwani Mh. Hassan Kambenga amesema hayo Mei 5 mwaka huu katika kikao cha baraza la madiwani ambapo amesema katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 3.082 zimeweza kutekeleza shughuli za maendeleo na kwamba ni Halmshauri chache zenye uwezo wa kujiendesha kwa kutegemea mapato yake kwa kuzingatia asilimia zilizowekwa kisheria kwani hapo awali ilikuwa ni vigumu kwa kujiendesha lakini kwa sasa inawezekana kutokana na ushirikiano uliopo kwa ngazi zote.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Katibu Tawala Yohana Kasitila akitoa nasaha katika baraza la madiwani lililofanyika Mei 5 mwaka huu amesema waheshimiwa madiwani wanao wajibu wa kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi na kuepusha ubadhilifu katika miradi kwenye maeneo yao lakini pia kuwa mstari wa mbele kuhakikisha inakamilika kwa wakati na inaleta tija katika jamii.
Kasitila amesema kuwa licha ya suala la usimamizi wa miradi lakini pia suala la utawala bora latika ngazi ya kata na vijiji limekuwa ni tatizo kutokana na vikao vingi vya kisheria kutofanyika licha ya kuwepo kwa viongozi husika katika maeneo hayo jambo ambalo limekuwa likisababisha malalamiko miongoni mwa wananchi ambapo kero za zimeonekana kutotatuliwa kiasi cha kupelekea wananchi hao kupeleka kero zao katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya kero ambazo zingetatuliwa na viongozi katika ngazi ya kata na vijiji hivyo amewataka ili shughuli za serikali ziweze kwenda kwa misingi ya utawala bora huku upande wa mapato akitaka kusimamiwa vema kwani eneo hilo la makusanyo ya mapato ya ndani hali yake iko chini.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Francis Kaunda amesema Halmashauri imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa na lengo la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa na wilaya jirani na kwa wasafiri mbalimbali kupitia sekta mbalimbali kama vile sekta ya afya, elimu, maji na nyinginezo na kuleta mafanikio makubwa kwa Halmashauri ambapo 40% ya mapato zinatumika katika miradi ya maendeleo na 60% kwenye matumizi mengine.
Kaunda amesema kuanzia mwaka 2015/2016 hadi Aprili 2020 Halmashauri imeweza kutumia jumla ya shilingi 3,082,935,593.24 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ambapo 10% imetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku 10% kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na 20% kwa ajili ya fedha za vijiji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa