Julai 10 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe S. Kebwe ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuendelea kutunza vyema rekodi waliyonayo na kupata hati inayoridhisha ambayo wameipata kwa miaka mitano mfululizo.
Kebwe amesema kuwa upatikanaji wa hati safi ama inayoridhisha ni ishara na alama nzuri ya mafanikio mazuri ambayo yameendelea kuonyesha utendaji na usimamizi mzuri washughuli mbalimbali katika Halmashauri jambo ambalo limeuletea sifa na heshima Mkoa wa Morogoro.
Aidha Kebwe amesema kuwa katika Mkoa wa Morogoro Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Morogoro zilizopata hati inayoridhisha ambapo Halmashauri ya Kilombero na Ulanga zimepata hati isiyoridhisha ambapo kupitia hati inayoridhisha ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuhakikisha mapato na matumizi sambamba na makusanyo yanafanyika inavyostahiki ili kuepuka kupata hati isiyoridhisha.
Sambamba na hayo Kebwe ameitaka Halmashauri ya Kilosa kuangalia kwa kina vyanzo vingine vipya vya mapato lengo ikiwa ni kuongeza mapato lakini pia ametoa wito kwa halmashauri kuwa na mashamba ya halmashauri pamoja na viwanda jambo litakalosaidia kuongeza mapato ya halmashauri.
Pamoja na hayo Dkt Kebwe amesitisitiza ufatiliaji wa madeni yote ya mashine za ukusanyaji mapato POS sambamba na madeni mbalimbali ambayo halmashauri inadai kutoka kwa watu mbalimbali yafuatiliwe na kulipwa mara moja.
Akisoma taarifa ya majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali ameridhishwa kuwa uandaaji wa hesabu hizo menejimenti ya Halmashauri Kilosa iliweza kuzingatia miongozo stahiki na hesabu haziakisi tafsiri potofu zilizotokana na wizi, ubadhirifu ama kasoro za kibinadamu ambapo pia ametoa maoni kuwa hesabu za mwaka za Halmashauri ya Kilosa zinaakisi hali halisi za shughuli za uendeshaji za kifedha na zile zisizo za kifedha na kuipatia hati inayoridhisha ikiwa ni mwendelezo wa miaka mitano mfululizo.
Aidha Asajile amesema kuwa Halmashauri inaendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti, kuziba mianya ya uwezekano wa kutokea kwa wizi na ubadhirifu lengo ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na utendaji wenye tija utakaoiwezesha Halmashauri kuendelea kupata hati zenye kuridhisha za ukaguzi mwaka hadi mwaka.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa