Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Kisena Mabuba ametoa rai kwa idara na vitengo kuiga mfano wa kiutendaji kutoka Idara ya Aafya ambayo imefanya vizuri kwa kipindi cha mwaka 2021 katika maeneo mbalimbali jambo lililopelekea matokeo chanya na kupata tuzo tatu ndani ya mkoa wa Morogoro.
Kisena ametoa rai hiyo wakati akipokea taarifa toka Idara ya Afya iliyotokana na kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi ambacho hufanyika kila mwaka ambapo kufuatia kikao hicho hutoa tathmini ya namna ambavyo halmashauri zote za mkoa wa Morogoro zilivyofanikisha kupunguza vifo hivyo.
Akitoa taarifa hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. George Kasibante amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeweza kupata tuzo 3 ambazo tuzo ya kwanza ikiwa ni kupunguza vifo vya uzazi kutoka 18/100,000 kwa mwaka 2020 hadi 6/100,000 kwa mwaka 2021, tuzo ya pili ikiwani kupunguza vifo vya watoto kutoka 37/100,000 kwa mwaka 2020 hadi vifo 16/100,000 kwa mwaka 2021 lakini pia Hospitali ya Wilaya ilipata zawadi ya kituo kilichosaidia kupunguza vifo.
Kasibante amesema kikao hicho hutoa fursa kwa kufanya tathmini na kujipima namna kila wilaya ilivyofanikisha katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na chini ya miaka mitano lakini pia hujadili namna bora ya kumvusha salama mama mjamzito kwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vile vifo vya watoto wachanga katika mkoa wa Morogoro.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa