Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha upatikanaji wa dola milioni 69 ambazo miongoni mwa shughuli zitakazofanyika kupitia fedha hizo ni kuboresha mbuga ya Mikumi ambapo kutakuwepo kiwanja cha ndege cha kisasa kitakachowezesha ongezeko watalii na pato kwa mbuga ya Mikumi na vijiji jirani.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mh. Dennis Londo wakati wa zoezi la uhamasishaji chanjo ya Uviko -19 na ushiriki wa sensa ambapo amesema idadi ya watalii itaongezeka kwa kasi ambapo wananchi watashiriki kikamilifu katika shughuli za kitalii kwa vijana kufadhiliwa kimasomo katika kozi zinazohusiana na shughuli za kitalii jambo litakalosaidia kukuza uchumi kiujumla.
Pamoja na hayo ameishukuru Serikali na Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha jimbo la Mikumi kwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari na msingi, nyumba ya watumishi wa afya na mashine ya mionzi itakayowekwa katika kituo cha afya Mikumi huku akitoa rai kwa wananchi kujitokeza katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo kupitia zoezi hilo itasaidia Serikali kupata idadi sahihi ya wananchi na kupanga mipango ya kuwahudumia wananchi kwa kadri ya idadi yao.
Katika kampeni hiyo ya uhamasishaji Mh Londo, Mkuu wa Wilaya na Katibu wa CCM Wilaya viongozi hao wameshiriki ujenzi wa chumba cha darasa katika kijiji cha Ihombwe ambapo Mkuu wa Wilaya Alhaji Majid Mwanga ametoa wito kwa wananchi ambao hawajachanja kuchukua hatua kwani yapo baadhi ya maeneo takwimu za uchanjaji haziridhishi kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi ambapo amewataka wananchi kutambua kuwa chanjo inasaidia kujikinga na Uviko-19 na ni salama na haina madhara yoyote, huku Katibu wa CCM Wilaya Comrade Shaban Mdoe akiwashauri ambao hawajachanja kuchukua hatua madhubuti za kuchanja kwa ajili ya musatakabali wa afya zao na kuwataka kuachana na propaganda ambazo hazina ukweli wowote kuhusu chanjo sambamba na kutoa rai kwa viongozi wa vijiji kuunga mkono juhudi za wenyeviti wa vitongoji pindi wanapoanzisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao..
Nao viongozi wa dini wametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo kwani ni salama na haina madhara yoyote huku wakibainisha kuwa lengo la chanjo ni kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya njema ambapo pia wamesisitiza ushiriki wa zoezi la sense ya watu na makazi pindi litakapoanza kwani sensa ni muhimu kwa ajili ya maandalizi ya bajeti na utoaji huduma katika jamii na maendeleo ya nchi kiujumla..
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa