Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imepokea miche 16,000 ya karafuu kutoka katika Taasisi ya TAHA na kuisambaza kwa baadhi ya shule ambapo shule hizo zitaanza kuvuna mazao hayo na kupata fedha zitakazosaidia kununua chakula kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula cha mchana mashuleni.
Hayo yameelezwa Aprili 24, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Elia Shemtoi katika kikao cha kujadili afua za lishe kwa kipindi cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambapo alieleza kuwa baada ya miaka minne, shule hizo zitaanza kuvuna mazao hayo ya kimkakati.
Pia Kikao hicho kimepitia mpango na matumizi ya fedha za lishe ambapo Ndg. Shemtoi alisisitiza kuwa hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata lishe bora na kutokomeza udumavu wa akili shuleni jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo yao ya kielimu na afya kwa ujumla.
Aidha, aliwasihi wazazi kutambua umuhimu wa lishe kwa watoto na kuchangia chakula shuleni huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa wazazi ni muhimu katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata mlo kamili shuleni, ambao unachangia katika ukuaji na maendeleo yao pia akiwahimiza walimu na viongozi wa shule kutumia maeneo ya kilimo yaliyopo shuleni kulima mazao ya chakula ili kuongeza upatikanaji wa lishe shuleni.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Lishe wa Wilaya ya Kilosa, Ndg. Elisha Kingu, alieleza kuwa licha ya asilimia 87.6 ya shule wilayani humo kutoa chakula shuleni, bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaokosa mlo wa mchana na kwamba hali hii inatokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uelewa mdogo wa wazazi kuhusu umuhimu wa kuchangia chakula shuleni.
Kwa upande wao, Maafisa Elimu wa Msingi na Sekondari walikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, wakieleza kuwa baadhi ya wazazi hawajitokezi kuchangia chakula kwa watoto wao. Hata hivyo, waliongeza kuwa baada ya msimu wa mavuno, wanatarajia idadi ya watoto wanaopata chakula shuleni itaongezeka, kutokana na wazazi kuwa na uwezo zaidi wa kuchangia.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Dismasi Mgao alihimiza shule zinazomiliki maeneo ya kilimo kutumia fursa hiyo kulima mazao mbalimbali na kupanda bustani za mboga mboga ambapo alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza upatikanaji wa chakula shuleni na kupunguza utegemezi kwa michango ya wazazi pekee.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa kuwataka wadau na jamii kusimamia na kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata lishe bora shuleni, ili kuboresha afya na maendeleo yao ya kielimu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa