Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Charles Kabeho amewataka watendaji wa umma kila mmoja kufanyakazi kwa bidii katika nafasi yake ili kuendana na kasi ya Kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli ya HAPA KAZI TU ili kuwaletea wananchi maendeleo kauli ambayo inasimamia sheria, taratibu, kanuni na weledi wa kazi.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ametoa maagizo hayo Julai 30 mwaka huu wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa Dodoma ambapo mbio hizo za Mwenge wa Uhuru wilayani Kilosa mkoani Morogoro zilimazika katika kata ya Lumuma na kukabidhiwa kimkoa katika Wilaya ya Mpwapwa katika jiji la Dodoma.
Kabeho amesema kuna baadhi ya watendaji wachache wa Serikali ambao bado hawajajua wajibu wao katika kutekeleza majukumu ya nafasi zao hivyo ametoa wito kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua watendaji kama hao ili wasiendelee kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na Serikali ya awamu ya tano.
Aidha, amewataka wananchi kuwekeza katika Elimu kwa kuwajibika kuwapeleka watoto wao shule kwa kuwagharimia kwa kuwapatia mahitaji ya msingi ya shule ikiwa ni pamoja sare za shule, kufuatilia taarifa za masomo yao na kushiriki kutoa michango inayohusu chakula cha watoto wawapo shuleni baada ya makubaliano ya wazazi wenyewe.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe muda mfupi kabla ya Makatibu Tawala wa Mikoa ya Dodoma na Morogoro kukabidhiana Mwenge wa Uhuru amewatakia wananchi wa Mkoa wa Dodoma unaoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Bilinith Mahenge matashi mema ya kutekeleza jukumu zito la kitaifa la Kukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa usalama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amesema Wilaya ya Kilosa imekamilisha Jukumu la Kukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa mafanikio makubwa ambapo miradi sita inayogharimu shilingi bilioni 2.3 imetembelewa na mwenge huo ikiwemo kuweka jiwe la msingi kituo cha afya Kidodi, ufunguzi wa mradi wa maji Mikumi, kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kusindika matunda Ihombwe, uzinduzi wa mabwawa ya samaki na kuona kilimo cha nyanya kwenye kitalu nyumba Ulaya Kibaoni pamoja na kuweka jiwe la msingi kituo cha mafuta Rudewa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa