Imeelezwa kuwa misitu mingi inaangamia ama kuteketea kutokana na umaskini ambapo hakuna namna misitu inaweza ikapona kutokana na kukithiri kwa ukataji miti kwa ajili ya mkaa ambao mahitaji yake ni makubwa katika maeneo mbalimbali hasa katika jiji la Dar es salaam ambapo watu wamekuwa wakikata miti bila kufuata utaratibu na kwamba licha ya mahitaji hayo makubwa ya mkaa hakuna sera ya Taifa inayotoa maelekezo ya namna gani mahitaji haya yaweze kufikiwa kwa njia endelevu bila kuathiri ikolojia na uchumi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa wakati wakurugenzi toka TAMISEMI walipotembelea wilayani Kilosa ikiwa ni ziara ya siku tatu katika vijiji vya Ulaya Mbuyuni, Ihombwe na Kitunduweta ili kujifunza nini kinachofanyika kupitia mradi wa mkaa endelevu kwa kushirikiana na TFS pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Kilosa ambapo amesema mradi wa mkaa endelevu unaofanya kazi katika vijiji 20 wilayani Kilosa lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanachoma mkaa katika njia endelevu kwani mkaa unatakiwa uzalishwe katika njia endelevu jambo litakalosaidia utunzaji wa misitu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Hifadhi ya Misitu ya Asili Tanzania Emmanuel Lyimo amesema kuwa kwa tafiti zilizofanywa na Wizara ya Maliasili Tanzania inapoteza kiasi cha misitu hekta zisizopungua laki nne kwa mwaka visababishi vikiwa ni kipato ambacho mwanadamu kubadilisha matumizi kutoka katika hali ya misitu na kuwa shamba kwa ajili ya kilimo pamoja na ufyekaji wa misitu kwa ajili ya mkaa ambapo ameshauri ili kukabiliana na hali hiyo ni vema serikali ikawa na misitu yake ya uvunaji na vijiji vikawa na misitu yake ya uvunaji ambayo itasimamiwa na kuiendeleza.
Aidha Lyimo ametoa ombi kwa TAMISEMI ijifunze muundo huo uliyotambulishwa na TFCG ili kuona namna unavyofanya kazi na kuusambaza nchi nzima kwani kupitia muundo huo utasaidia vijiji kutenga maeneo na kunufaika na misitu kwa kutumia rasilimali za hapa hapa nchini ambapo vijiji vitaweza kunufaika na kipato kinachotokana na misitu ili jamii iweze kunufaika ikiwemo usimamizi wa fedha kwani vijiji vingi vilivyopo katika mradi hali ya misitu ni nzuri kuliko ya vijiji ambavyo haviko kwenye mradi.
Naye Mkurugenzi wa Serikali za mitaa Dkt. Charles E. Mhina kwa niaba ya wakurugenzi wenzake toka TAMISEMI amesema kuwa idara yake inapotembelea Kilosa imelenga kuangalia namna Wilaya inavyotekeleza mradi, namna inavyotunza misitu kwa kuwa na unyevunyevu mzuri lakini pia ziara yao imekusudia kupokea changamoto na kuziwasilisha serikali sambamba na kuishauri juu ya changamoto mbalimbali zinazoikumbuka wilaya lakini pia namna ambavyo Halmashauri ingependa kupokea maelekezo ya kisera.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Hassan S. Mkopi amesema kuwa mradi wa mkaa endelevu umekuwa wa manufaa kwani umekuwa ni shirikishi na vijiji vyenye mradi wananchi wamenufaika kwa kupata ofisi za vijiji, Halmashauri imekuwa ikipata mapato kupitia misitu, ujenzi wa madarasa, wananchi wamefanikiwa kulipia CHF, kipato kimeongezeka kwa wananchi, kuna ongezeko la kipato ka ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii na Halmashauri na kuboresha afya ya jamii, kuboresha, pamoja na hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mambambale amesema kuwa Halmashauri haiwanyang’anyi wananchi chochote wanaojihusisha na mradi wa mkaa endelevu bali inatekeleza sheria za nchi kwa kutoa utaratibu ambao ni sahihi kwa wananchi kuufuata.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa