Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amewataka wamiliki wa nyumba za kulala wa wageni almaarufu gesti kutambua kuwa ni wajibu wa kila mmiliki wa gesti kulipa tozo stahiki kwani tozo (kodi) hizo ni kwa mujibu wa sheria ambazo hutungwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwambambale amesema hayo wakati wa kikao cha majadiliano baina yake na wamiliki wa gesti ambao walitoa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika biashara zao ikiwemo ombi la wamiliki kutaka kupunguziwa bei ya vitabu vya kupokelea wageni ambavyo awali ilikuwa ni shilingi 10,000 lakini baada ya majadaliano hayo bei imefikia kuwa shilingi 5,000/ kwa kila kitabu ambavyo vinapatikana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika ofisi za biashara.
Aidha Mwambambale amewataka wamiliki hao kutambua kuwa uwepo wa vitabu hivyo ni muhimu kwani vitasaidia kuwa na udhibiti mzuri wa mapato kwa upande wa halmashauri na wamiliki ambao gesti hizo huwa chini ya wasimamizi wanaoajiriwa na wamiliki hao, hivyo kila mmiliki ahakikishe gesti yake inakuwa na vitabu hivyo vyenye mfumo mmoja ulio katika ubora pindi ifikapo tarehe 01/10/2018.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri Edward Kutandikila amewataka wamiliki hao kutii sheria bila shuruti na kuheshimu sheria zilizowekwa na kuzifuata ikiwemo kulipa tozo husika kwa wakati muafaka ili kuepuka kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo ulipaji wa leseni kwa wakati ili kuepuka kulipa faini.
Sambamba na hayo wamiliki wa gesti wameiomba ofisi ya Mkurugenzi kuwatazama kwa jicho la karibu kwa kuwasaidia kupunguza gharama za nauli wanazolipia kuja Kilosa na kurudi maeneo yao kwa kuweka vituo vya muda vya watendaji toka ofisi ya biashara katika maeneo yao ili kukusanya tozo husika na kuziwasilisha, pia wamemkabidhi Mkurugenzi huyo katiba ya wafanyabiashara ikiwa ni sehemu ya kuonyesha ushirikiano wao kwa uongozi huo wa Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa