Imeelezwa kuwa mfumo dume, mila na desturi kandamizi, ukeketaji, kuvunjika kwa baadhi ya mila zilizokuwa zinasaidia ulinzi kwa watoto, matumizi ya madawa ya kulevya na pombe, umasikini ni miongoni mwa mambo yanayosababisha ukatili miongoni mwa jamii.
Hayo yamebainishwa na Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kilosa Tumaini Geugeu wakati wa kikao cha wadau wa masuala ya watoto ambapo amesema kuwa suala la ukatili linamgusa kila mtu, hivyo jamii kiujumla inapaswa kupinga ukatili ili jamii iweze kukaa salama.
Akieleza zaidi kuhusu ukatili Guegeu amesema jamii itambue kuwa ukatili uko wa aina nne ambapo aina ya kwanza ya ukatili ni ukatili wa kingono ambapo baadhi ya familia baba, mama na watoto hulala chumba kimoja huku watoto wakishuhudia matendo yote yanayoendelea jambo ambalo huzaa ukatili kwa watoto na kusababisha mimba za utotoni, ukatili wa aina ya pili ni ukatili wa kimwili kama vile vipigo, ukatili wa aina ya tatu ni ukatili wa kihisia ikiwemo maneno ya kuumiza na kudhalilishwa na mwisho ni ukatili wa kiuchumi ikiwemo kutelekezwa na kunyimwa fursa za kiuchumi.
Chanzo kikubwa cha ukatili katika jamii kwa asilimia kubwa huchangiwa na malezi yasiyofaa kwa watoto ambapo hupelekea watoto kadri wanavyokuwa kiumri hujikuta katika tabia zisizofaa ambazo huzaa matendo ya kikatili kama vile ubakaji, vipigo, kunyimwa haki ya kujitetea na kueleza ukweli dhidi ya vitendo viovu ambavyo wazazi ama ndugu huwafanyia watoto, wanawake na hata wanaume kwani ukatili sio kwa wanawake na watoto tu bali hata wanaume.
Jamii inapaswa kufahamu kuwa madhara ya ukatili ni makubwa ikiwemo ongezeko la watoto wa mitaani, ongezeko la wagonjwa waliotelekezwa hasa wazee, migogoro ya ndoa na talaka, maambukizi ya magonjwa ya zinaa, visasi, vifo, ndoa za utotoni, mimba za utotoni pamoja na mendeleo duni ya kiuchumi.
Aidha wadau walioshiriki kikao hicho kwa kushirikiana na Afisa Ustawi wa Jamii wametoa wito kwa wazazi na jamii nzima kutoa ushirikiano katika kesi mbalimbali zinazojitokeza zinazohusu ukatili kwani imebainika kuwa baadhi ya wazazi kwa asilimia kubwa wamekuwa chanzo kikubwa cha kuendeleza ukatili kwa kutotoa ushirikiano wa kutosha katika kesi hizo na kusababisha haki kutotendeka kwa mtu aliyefanyiwa ukatili.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa