Kutokuwepo kwa utawala bora kwa viongozi kuanzia ngazi ya vijiji hadi ngazi ya juu sambamba na kutowajibika inavyostahiki kwa mujibu wa mfumo wa serikali ni miongoni mwa changamoto zilizochangia kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi pamoja na umaskini.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati wa kikao chake na wazee maarufu, wafanyabiashara, viongozi wa dini, waheshimiwa madiwani wa kata zote za mjini pamoja na watendaji wa kata lengo likiwa ni kujadili hali ya maendeleo wilayani kilosa.
Mgoyi amesema kuwa miaka michache ilopita hali ya kiwilaya haikuwa sawa kutokana na changamoto tajwa ambazo kwa sasa kwa asilimia kubwa zimepungua ambapo amesema kuwa viongozi walikuwa wakiangalia maslahi binafsi jambo ambalo kwa sasa limeaanza kufanyiwa kazi na hali imeanza kuwa shwari
Aidha mgoyi amewataka washiriki wa kikao hicho kutoa mawazo yao kwa namna gani Kilosa inavyoweza kuwa na maendeleo kwani kwa mazingira yaliyopo mabadiliko yanawezekana kwani viongozi wa dini wapo , wanasiasa vilevile ambao wanaweza kuchangia mabadiliko katika sekta mbalimbali.
Wakitoa michango yao kwa niaba ya wenzao mzee Nchimbi Nackam na mzee Antony Fuime wamesema kuwa chanzo cha migogoro ni ukosefu wa umoja wa kutafuta maendeleo sababu kubwa ikiwa ni ubinafsi katikati ya watu, wanasiasa kukosa nguvu ya ushawishi katika kushawishi wananchi kuchangia maendeleo badala yake siasa zimekuwa zikichukua nafasi kubwa badala ya maendeleo, sambamba na hayo amewaomba viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuhamasisha waumini wao kutumia vema fursa za maendeleo zinazojitokeza.
Naye mzee Peter Thomas pamoja na mzee Raphael Chayeka wameshauri kuwepo kwa zao la kudumu la kutambulisha zao hilo ambalo litakuwa likilimwa na jamii ya watu wa Kilosa ambalo litalimwa kiasi kikubwa na kutafutiwa soko hasa katika kukuza uchumi wa Kilosa, Halmashauri itunge sheria ndogo itakayowalazimisha wazazi kuchangia chakula kwa ajili ya watoto, lakini kuwe na suala la uwajibikaji kwa watumishi ambapo kila mtu awajibike kwa ngazi yake .
Aidha wazee hao wametaka ujenzi wa mji usijengwe kiholela kwani ujenzi holela unasababisha kutokuwa na miundombinu iliyo bora, lakini pia wameomba ufanyike mchakato kwa ajili ya tuta la mto Mkondoa ambalo kwa kiwango kikubwa limekuwa likileta athari kwa wananchi na kurudisha nyuma maendeleo huku upande wa CHF iliyoboresha wamesema baadhi ya dawa muhimu zimekuwa hazipatikani wakati upande wa elimu wameshauri sekta ya elimu iweke namna ya kurudisha elimu kwa watu wazima sambamba na wazazi kuwa kipaumbele katika kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kuwa katika mazingira mazuri na salama kwao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Hassan Mkopi amesema kuwa mawazo, ushauri na changamoto zilizotolewa watazifanyia kazi ambapo pia amewataka washiriki wa kikao hicho kushiriki katika vikao vya vijiji kwenye maeneo wanakotoka kwani maendeleo huanzia ngazi ya chini, hivyo ushiriki wao unaweza kuongeza tija katika kuleta maendeleo lakini pia amemuomba Mkuu wa Wilaya kufikisha salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa awamu ya Tano kwa fedha ambazo Serikali imekuwa ikizitoa kwaajili ya maendeleo ya Wilaya ya Kilosa.
Pamoja na hayo yote Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Rwegerera Katabaro kwa niaba ya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ameahidi kuyafanyia kazi yale yote yanayohusu watalaam wa halmashauri kwa kuhakikisha wanafanya majukumu yao kwa mujibu wa taratibu za kazi zinavyowataka na kuwajibika ipasavyo huku Mkuu wa Jeshi la Polisi Kilosa Mayenga Mapalala amesema kwa upande wa Jeshi la Polisi watafanya wajibu wao na kuomba kupatiwa taarifa zote za kiuhalifu ili waweze kuzifanyia kazi kwani ni wajibu wao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa