Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali ikiwa ni pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za miradi hiyo lakini pia kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa Machi 29, 2025 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Halima Mdee (Mbunge) wakati wa kamati hiyo ilipotembelea miradi miwili ambayo ni ujenzi wa mabweni matatu, madarasa saba na vyoo matundu kumi pamoja na uzio vyenye thamani ya shilingi 612,000,000/= fedha kutoka serikali kuu na shilingi 215,000,000/= kutoka mapato ya ndani katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Dakawa lakini pia mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala wenye thamani ya shilingi bilioni 3.6
Akiwasilisha majumuisho ya ziara hiyo, Mhe. Noah Lemburis Mollel (Mbunge) ameitaka Halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa kwa mjibu wa miongozo iliyotolewa na Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa (TAMISEMI).
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Atupele Mwambene ameihakikishia kamati ya LAAC kuwa mapungufu yaliyobainishwa kwenye ziara hiyo kuwa yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi na miongozo kwa watendaji walioko chini ya TAMISEMI wakati wa Utekelezaji wa Miradi hiyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea miradi hiyo na kutoa maelekezo na maboresho kwenye miradi hiyo na kuahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itashirikiana na Halmashauri katika uboreshaji wa miradi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka naye ameihakikishia kamati hiyo kuwa ataendelea kuisimamia Halmashauri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kufikia azma ya serikali ya kuwaletea huduma na maendeleo wananchi.
Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mhe. Douglas Mwigumila ambaye ni Diwani wa Kata ya Dumila ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya ya Kilosa.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Beatrice Mwinuka amefafanua kuwa pamoja na mapungufu pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradihiyo, Halamshauri imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha miradi inakamilika ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi hiyo, kuwateua wasimamizi maalumu wa miradi hiyo lakini pia kuwasimamia wakandarasi wanaojenga miradi hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa