Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Kangi Lugola ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuhakikisha zinasimamia uwepo wa ulinzi na usalama na kushughulikia ishara zozote za uvunjifu wa amani ikiwemo maandamano na mikutano ya ndani ya vyama vya kisiasa yenye lengo la kumkashifu Rais ama kuhatarisha usalama wa Mikoa na Wilaya kiujumla.
Kangi ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara wilayani Kilosa ambapo amesema kuwa licha ya uwepo wa amani na usalama uliopo nchini bado amani na usalama unahitaji kuendelea kudumishwa hivyo ni vema kamati zikadumu katika kudumisha hali ya kiusalama kwa wilaya nzima ya Kilosa.
Akizungumzia juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya Tano Kangi amesema kuwa Rais amekuwa akifanya mambo mengi yenye tija kwa watanzania waliompa dhamana ya kuongoza nchi ikiwemo kudumisha usalama wa nchi, na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa ya kudumisha amani kwani nchi inapokosa amani hakuna jambo lolote la kimaendeleo linaloweza kuendelea.
Kwa upande wa migogoro ya ardhi Kangi amesema mahali popote penye migogoro ya aina hiyo ni dalili za uvunjifu wa amani na kwamba yoyote atakayebainika kusababisha uvunjifu wa amani kamati za ulinzi na usalama zisisite kumchukulia hatua sambamba na kuwachukulia hatua wote wanaohusika kumtukana Rais ama kukashifu viongozi na kwamba mikutano ya kisiasa ilipigwa marufuku na mheshimiwa rais badala yake muda huo utumike kwa ajili ya wananchi kujitafutia maendeleo.
Kangi amewaonya wananchi kutumia kutotumika kuwaficha wahamiaji haramu kwani idara ya uhamiaji itakapowabaini itawashughulikia huku akisisitiza idara ya vitambulisho NIDA kuwapa vitambulisho wale wanaostahili na amewataka wananchi kuepuka vitendo vya wizi hasa katika ujenzi wa reli ya kisasa unaondelea na ametaka wazawa wa Kilosa kupewa kipaumbele katika ajira.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi kuwa na nidhamu na kuwahudumia wananchi kwa haki na kuzingatia sheria ambapo amepiga marufuku kukamatwa hovyo kwa boda boda pasipokuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani na kwamba boda boda wapewe elimu badala ya kuwavizia na kuwapiga faini na amesisitiza pikipiki zinazopaswa kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi ni zile zinazohusika na uhalifu, zinazohusika kwenye ajali na zinazookotwa zisizo na wenyewe.
Aidha kwa upande wa mgogoro wa shamba la Mauzi Estate Kangi amewaagiza wananchi wanaodai kuwa wamepewa eneo hilo ili walilime kuandaa nyaraka zinazoonyesha wamepewa eneo hilo, pili amemtaka mmiliki/mrithi wa shamba hilo Bw. Aris Daimon kuandaa nyaraka zinazoonyesha umiliki wa shamba hilo sambamba na Halmashauri kuandaa nyaraka zenye maelezo ya shamba hilo na kuziwakilisha kwake ifikapo tarehe 15/03/2019 atakapotembelea tena kata ya Kimamba ili mgogoro huo uweze kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na waziri wa Ardhi ili kuepuka uvunjifu wa amani.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa