Kila mwaka ifikapo tarehe 16 juni Tanzania inaungana na Nchi zingine za afrika kuadhimisha siku ya mtoto wa afrika, ambapo chimbuko la maadhimisho hayo ni azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya kusini waliouawa juni 16, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Hayo yameelezwa na katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Salome Mkinga ambaye alikuwa mgeni ramsi akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu shaka juni 16 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ambapo kiwilaya yaliyofanyika katika kata ya Magomeni kwenye viwanja vya shule ya msingi Lamulilo.
Katibu Tawala huyo ameitaka siku hiyo kutumika katika kukumbushana, kuhamasishana, na kupeana taarifa juu ya changamoto zinazowakabili watoto ikiwemo ukatili wa aina mbalimbali kama vile ulawiti, ubakaji, utumikishwaji katika ajira hatarishi, ndoa na mimba za utotoni,ukeketaji na ukatili wa mitandaoni.
Mkinga amesema ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali imesaini na kuridhia mikataba ya kimataifa kuhusu haki ya mtoto ya mwaka 1991,na mkataba wa Afrika wa haki na ustawi wa mtoto ya mwaka 2003 ambayo yote kwa pamoja imetoa miongozo ya kusimamia ulinzi na haki kwa mtoto.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Alto Mbikiye amesema kuwa maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidigitali” inawataka wazazi, Walezi , Serikali na wadau wengine kuzingatia haki za watoto ikiwa ni pamoja na malezi mazuri,matunzo na ulinzi kwa usalama wa mtoto.
Kwa upande wake Afande Hemedy Chabu kutoka Dawati la jinsia Polisi Wilaya ya Kilosa amewakumbusha wazazi kufuatilia kwa ukaribu na kukagua mienendo ya watoto ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili huku akiwaasa kutoa taarifa haraka katika vitengo husika pindi wanapobaini kutokea kwa vitendo hivyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa