Maafisa kilimo wilayani Kilosa wametakiwa kutoa ushirikiano mkubwa wa kutoa taarifa pindi inapojitokeza jaribio la utoroshwaji wa mazao unaofanywa na wanunuzi wa mazao katika kata na vijiji vyao ambao wamekuwa na hulka ya kukwepa kulipa ushuru kwa mazao wanayonunua kwa wakulima kwa lengo la kuyasafirisha bure.
Rai hiyo imetolewa Novemba 21 mwaka huu na Mkuu wa idara ya Kilimo Elina Danstan wakati wa kikao kazi cha maafisa kilimo ngazi ya wilaya, kata na vijiji ambapo licha ya kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha kilimo wilayani Kilosa pia amewataka maafisa hao kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za utoroshwaji wa mazao kwani wilaya imekuwa ikipoteza pato kutokana na wanunuzi wachache ambao wamekuwa wakikwepa kulipa ushuru.
Katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo uwajibikaji wa maafisa ugani kwa kuhakikisha wanakuwa na daftari la orodha ya wakulima, daftrari la huduma za ugani, ujazaji wa opras, ambapo pia wametakiwa kuwa na taarifa za tathmini ya hali ya chakula kwenye maeneo yao lakini pia kutekeleza mpango mkakati wa kilimo msimu wa 2019/2020 kwa kuyatambua na kuyapa kipaumbele mazao ya kipaumbeke ikiwemo pamba, korosho, miwa, mkonge na muhogo sambamba na mazao muhimu ya chakula ikiwemo mahindi, mpunga na muhogo.
Pamoja na hayo wametakiwa kuhakikisha katika maeneo yao wanakuwa na mshamba darasa ili kutoa elimu kwa wakulima wengi, kusimamia matumizi ya kanuni boara za kilimo, kusimamia kalenda ya mazao kwenye skimu za umwagiliaji na usimamizi wa zana bora za kilimo lakni pia wametakiwa kuwa na rejista ya matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji na jinsi ilivyotatuliwa sambamba na kuwa na mfumo mzuri wa kufanya tahmini ya mazao yaliyoharibiwa na mifugo.
Naye Afisa Utumishi na Utawala Wilaya Noel Abel ametoa onyo kwa maafisa hao kuacha mara moja tabia ya kuwatoza wakulima huduma za ugani kwani baadhi ya wakulima wamekuwa wakiwalalamikia maafisa hao kuwatoza huduma ikiwemo kufanyiwa thmini na huduma nyinginezo huku akiwataka watumishi wote kutambua upandaji wa madaraja/vyeo hutegemea na muundo wa kada husika kwani vipo vigezo vinavyomfanya mtu apande daraja/ cheo ikiwemo ujazaji wa opras, kutimiza miaka mitatu katika cheo husika, kutambua muundo wa cheo unavyoeleza na taratibu zake, pia amewataka maafisa hao kuwepo katika vituo vya kazi kwani baadhi yao wamekuwa watoro kazini ambapo amesema atayebainika kutokuwepo kazini bila ruhusa kwa zaidi ya siku tano atasimamishiwa mshahara.
Sambamba na hayo maafisa hao wameiomba Serikali iitazame sekta ya kilimo kwa jicho la tatu kwa kutoa ruzuku kwa wakulima hasa wakulima wadogo ili kuwainua katika kilimo kwani sekta ya kilimo ndio inayotoa pato kubwa, hivyo inahitaji kuinuliwa zaidi huku wakitoa rai kwa Halmashauri kuwawezesha maafisa kilimo kuunda mashamba darasa katika kila kata huku wakiuomba uongozi wa wilaya kukaa na wadau mbalimbali na kuwapa elimu kuwa wasitumie siasa katika kampeni za kuhamasisha wakulima katika kulima mazao flani flani kwani ahadi mbalimbali zimekuwa zikitolewa pasipo kutekelezwa jambo linalowawia ugumu katika utoaji huduma kwa wakulima.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa